1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabaki ya ndege ya AirAsia yapatikana

30 Desemba 2014

Waokoaji wa Indonesia wameiona miili na mizigo ikielea majini katika kisiwa cha Borneo maafisa wamethibitisha kuwa mabaki yaliyoonekana ni ya ndege ya AirAsia iliyotoweka siku mbili zilizopita ikiwa na watu 162.

https://p.dw.com/p/1ECIT
AirAsia Airbus 320-200 vermisst 30.12.2014
Picha: Bay Ismoyo/AFP/Getty Images

Maafisa wa Indonesia wamesema mapema leo kuwa wameiona miili sita ya ndege ya AirAsia na wametoa miili mitatu kutoka baharini. Miili hiyo imepatikana katika bahari ya Java karibu kilomita 10 kutoka eneo ambalo ndege hiyo nambari QZ 8501 ilifanya mawasilino ya mwisho na waongozaji wa safari za ndege. Ndege hiyo iliyokuwa na watu 162 ilitoweka Jumapili iliyopita ikiwa safarini kutoka Surabaya, Indonesia kuelekea Singapore baada ya kukabiliwa na hali mbaya ya hewa.

Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Uokozi amewaambia waandishi karibu na mji ulio karibu wa Pangkalan Bun,kuwa miili mitatu iliyopatikana, ilikuwa imevimba lakini katika hali nzuri, na imepelekwa kwenye meli ya jeshi la majini la Indonesia.

AirAsia Airbus 320-200 vermisst 30.12.2014 Radar
Afisa wa hali ya hewa akionyesha sehemu ilikokabiliwa na matatizo ndege ya AirAsiaPicha: imago/Xinhua

Picha zilizorushwa kwenye televisheni ya Indonesia zilionesha miili kadhaa ya watu ikielea baharini. Waokoaji kisha wakateremshwa kwa kamba kutoka kwenye helikopta na kuiopoa miili hiyo. Mkurugenzi mkuu wa Shirika la AirAsia nchini Indonesia Sunu Widyatmoko amewaambia waandishi wa habari mjini Surabaya ambako ndege hiyo iliondoka siku ya Jumapili, kuwa ndege iliyowabeba jamaa na familia za wahanga wa ajali hiyo imepelekwa katika eneo hilo.

Msemaji wa jeshi la majini amesema mlango wa ndege hiyo, vifaa vya oksijeni na pia vimepatikana na kuondolewa majini ili kufanyiwa uchunguzi. Shughuli hiyo ya uokozi imekuja saa chache baada ya vipande kadhaa vya rangi nyekundu, nyeupe na nyeusi kuonekana katika bahari ya Java karibu na kisiwa cha Borneo.

Karibu meli 30 na ndege 21 kutoka Indonesia, Australia, Malaysia, Singapore, Korea Kusini na Marekani zinahusika katika shughuli hiyo ya uokozi. Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya AirAsia Tony Fernandes ametuma risala za rambirambi akisema kwenye Twitter, kuwa moyo wake umejaa huzuni kwa familia zote zilizohusika na ajali hiyo.

Wakati hayo yakijiri, Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Uokozi nchini Indonesia amesema ndege ya kijeshi imegundua “kivuli” chini y abahari ambacho kinaaminika kuwa cha nddge hiyo ya AirAsia.

Bambang Soelistyo amewaambia waandishi wa habari kuwa shughuli za utafutaji sasa zinaendelea katika eneo ambako kivuli hicho pamoja na mabaki yamepatikana, karibu kilomita 160 Kusini Magharibi ya mji wa Pangkalan Bun.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga