1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko Bangladesh

Mohammed Abdul-Rahman23 Agosti 2007

Serikali ya mpito nchini Bangladesh yajaribu kutuliza vurugu, kwa kutangaza siku ya mapumziko.

https://p.dw.com/p/CH9D
Kiongozi wa serikali ya mpito Fakhruddin Ahmed
Kiongozi wa serikali ya mpito Fakhruddin AhmedPicha: DW

Serikali inayoungwa mkono na jeshi nchini Bangladesh leo imetangaza siku ya mapumziko ikiwa ni kujaribu kumaliza mvutano na machafuko ya siku tatu yaliosambaa kutoka chuo kikuu cha Dhaka hadi miji mengine nchini humo. Jana kiongozi wa serikali ya mpito Fakhruddin Ahmed alitangaza kwamba amri ya kutotoka nje ili kuzuwia kile alichokiita “ vurugu na ukosefu wa utawala wa kisheria,” itaendelea hadi itakapotangazwa baadae.

Bangladesh imekua katika katika amri ya hali ya hatari tangu Januari, pale serikali ya mpito ilipochukua madaraka baada ya miezi kadhaa ya machafuko na hali mgogoro wa kisiasa kuhusiana na madai ya udanganyifu katika upigaji kura.

Wakati amri ya kutotoka nje ilipoanza kufanya kazi baada ya machafuko ya wanafunzi ya siku tatu mfululizo wiki hii, simu zote za mkononi zilisita kufanya kazi kwa sababu ya kusimamishwa mitandao yote ya mawasiliano katika kile kilichotajwa na shirika la habari la Bagladesh (UNB) kuwa ni amri ya serikali.

Karibu watu 60 wakiwemo baadhi ya waandishi habari walikamatawa, wakati watu walipokua wakikimbilia majumbani na mitaa ikiwa mitupu. 35 kati yao, wakiwemo waandishi habari 12, waliachiwa huru kwa dhamana wakati wengine wamebakia rumande. Kulikua na taarifa za kupigwa waandishi habari kiasi ya wawili na askari wa usalama, licha ya kwamba walijitambulisha kwa kutoa vitambulisho vyao.

Polisi wamweka vituo vya ukaguzi katika barabara zote za mji mkuu Dhaka na maelfu ya abiria waliripotiwa kukwama katika uwanja wa ndege wa mji huo mkuu na biashara zote zilifungwa.

Waziri mkuu Ahmed alisema amri ya kutotoka nje kuanzia magharibi hadi alfajiri ina lengwa katika kulinda mali za watu na kuzuwia vitendo vya ukiukaji sheria na akasisitiza kwamba hatua hiyo ni ya muda tu. Katika hotuba yake kwa taifa kwa njia ya Televisheni Bw Ahmed aliyataja machafuko hayo kuwa ni “Njama”

Serikali imetoa wito kwa raia kuwa watulivu, lakini wakati huo huo ikiwashutumu wafanyaji fujo kwa kuyateka nyara maandamano ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Dhaka kuwa vurugu na machafuko bila ya sababu za mingi. Wanafunzi walikua wakiwataka Wanajeshi kulihama eneo la chuo kikuu.

Licha ya kituo cha kijeshi chuoni umo kufungwa mapema Jumatano, mapigano yalizagaa na kuendelea hapa na pale . Chuo kikuu cha Dhaka kikiwa na wanafunzi 40,000 leo kilikua kitupu, baada ya serikali kukifunga pamoja na vyuo vyengine, na polisi na wanajeshi wamekua wakipiga doria katika mitaa ya karibu.

Serikali ya mpito imekua ikiungwa mkono na umma. Tangu ilipoiingia madarakani, baada ya miongo karibu miwili ya tawala za wanasiasa waliogubikwa na shutuma za rushwa. Kufuatia fujo hizo na maandamano ya wanafunzi, wachambuzi nchini Bangladesh wameitaka serikali kutoyapuuza na kuyafuatilia kwa makini matukio hayo.Serikali kwa upande mwengine imevionya vyombo vya habari kutochapisha au kutangaza habari zinazoweza kuchochea ghasia.

Mtu mmoja aliuwawa na karibu wengine 300 kujeruhiwa katiaka mapigano kati ya polisi na wanafunzi waliungwa mkono na raia wengine , wakati wa ghasia za hivi karibuni