1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko mjini Stuttgart dhidi ya ujenzi wa kituo kikubwa cha safari za reli

Oumilkher Hamidou1 Oktoba 2010

Watu wasiopungua 100 wamejeruhiwa polisi ilipotumia mipira ya maji na gesi za kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji mjini Stuttgart

https://p.dw.com/p/PRrE
Machafuko ya Schlossgarten polisi walipotaka kuingia katika bustani hiyoPicha: dpad

Polisi katika mji wa kusini magharibi wa Ujerumani-Stuttgart wametumia mipira ya maji jana kuwatawanya waandamanaji wanaopinga mradi wa ujenzi wa kituo kikubwa kabisa cha safari za reli kati eneo la kati la mji huo.Kansela Angela Merkel ametoa mwito wa utulivu.

Machafuko yaliripuka kati ya waandamanaji na polisi ambao baadhi yao walipanda farasi na kuingia katika bustani ya Schlossgarten ambako miti zaidi ya 25 inapangwa kukatwa hadi february mwakani ili kufungua njia ya kujengwa kituo kikubwa cha sarafi za reli kinachojulikana kama "Stuttgart 21.

Mradi huo umezusha ghadhabu miongoni mwa wakaazi wa jimbo la kusini magharibi ya Ujerumani-Baden-Wurtemberg.Wapinzani wa mradi huo wanalalamika pia jinsi polisi walivyotumia marungu,mipira ya maji na gesi za kutoa machozi dhidi yao.Kwa mujibu wa polisi watu zaidi ya mia moja wamejeruhiwa,lakini waandamanaji wanadai zaidi ya watu 300 wamejeruhiwa.

"Polisi inawapiga watu kwenye uso.Kuna walioumizwa kwenye kichwa,kuna wenye majaraha shingoni na watu wengi pia wana matatizo ya macho kwasababu polisi wametumia gesi za kutoa machozi."

Maandamano yamekuwa yakiitishwa takriban kila wiki tangu mwezi mmoja uliopita kupinga mradi huo unaotajikana kuwa mmojwapao wa miradi mikubwa kabisa barani Ulaya na ambao utagharimu zaidi ya Euro bilioni sabaa kwa muda wa miaka tisaa.

Maandamano hayo yanachukua sura ya lawama dhidi ya serikali kuu ya muungano wa vyama ndugu vya CDU/CSU na waliberali wa FDP mjini Berlin.

NO FLASH Stuttgart 21 Demonstration
Waandamanaji wajikinga dhidi ya mabomba ya maji ya polisiPicha: AP

Kansela Angela Merkel ametoa mwito wa utulivu akisema tunanukuu:"nataraji maandamano kama hayo yatafanyika bila ya matumizi ya nguvu."Mwisho wa kumnukuu kansela Angela Merkel.

Malalamiko ya wananchi dhidi ya mradi huo yanawafaidisha walinzi wa mazingira na ahuenda yakatumiwa katika kampeni za uchaguzi wa bunge unaopangwa kuzitishwa March mwakani katika jimbo hilo la kusini magharibi ya Ujerumani.Kwa mujibu wa utafiti wa maoni ya umma,chama cha CDU cha kansela Angela Merkel kinachoongoza serikali ya jimbo hilo tangu mwaka 1953 kinakabiliwa na hatari ya kushindwa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters,Afp,dpa

Mpitiaji:Josephat Charo