1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko ya Sudan yaongeza hofu ya vita

25 Aprili 2012

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameshutumu mashambulio ya angani yanayofanywa na Sudan katika mipaka ya Sudan Kusini, na akiwataka viongozi wa nchi hizo mbili kuwacha kujiingiza katika vita.

https://p.dw.com/p/14jyY
A man gestures at a market burnt in an air strike by the Sudanese air force in Rubkona near Bentiu April 23, 2012. Sudanese warplanes carried out air strikes on South Sudan on Monday, killing three people near the southern oil town of Bentiu, residents and military officials said, three days after South Sudan pulled out of a disputed oil field. REUTERS/Goran Tomasevic (SOUTH SUDAN - Tags: CIVIL UNREST POLITICS CONFLICT)
Sudan Südsudan Rubkona Markt Bombardement Hass ZornPicha: Reuters

Lakini wakati hayo yakiendelea, Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir hii leo anaanza ziara ya kiserikali nchini China, ambako atakutana na mwenyeji wake Hu Jintao. Sudan na Sudan Kusini zimekuwa zikipigana katika miezi ya hivi karibuni katika eeno lao mpaka wao lililo na utajiri wa mafuta, hali iliyoibua hofu kutoka wka jamii ya kimataifa  kuhusu uwezekano wa kuzuka vita.

Wito wa Ban kutaka utulivu umejiri baada ya rais wa Sudan Omar al-Bashir kufuta uwezekano wowote wa kufanya mazungumzo na hasimu wake wa Kusini Salva Kiir, ambaye yuko mjini Beijing, kutafuta uungaji mkono kutoka wka China ambaye ni mshirika wa tangu jadi wa Sudan.

Rais wa Sudan Omar al-Bashir anasakwa na mahakama ya ICC
Rais wa Sudan Omar al-Bashir anasakwa na mahakama ya ICCPicha: Reuters

Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Eduardo del Buey amesema Ban amekariri kuwa hakuwezi kuwa na suluhu ya kijeshi katika mizozo baina ya Sudan na Sudan Kusini. Amemtaka rais Bashir na rais Kiir kuwacha kujiingiza katika vita na badala yake kurejea  katika meza ya mazungumzo haraka iwezekenavyo.

Sudan Kusini ilisema Jumapili kuwa imeviondoa vikosi vyake vyote kutoka jimbo linalogombaniwa la Heglig, lakini mashambulizi ya angani yalifanywa jana Jumatatu Bentiu, ambao ni mji mkuu wa jimbo la upande wa Kusini la Unity.

Kiir yuko mjini Beijing

Salva Kiir ambaye yuko ziarani China anatarajiwa kukutana na mwenzake wa China Hu Jintao baadaye leo katika mazungumzo ambayo huenda yakaulenga mzozo huo kati ya Sudan Kusini na Sudan. China imekuwa rafiki mkubwa wa Sudan na pia mshirika mkuu wa kiuchumi wa Sudan, ambapo imeisaidia kuwa muuzaji mkubwa wa mafuta.

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini Salva KiirPicha: picture-alliance/dpa

Lakini kujitenga kwa Upande wa Kusini kutoka Kaskazini mwezi Julai mwaka wa 2011, pamoja na machafuko ya hivi karibuni, kumeilazimu China kutokuwa na msimamo wa wazi katika kujaribu kuendelea kuiunga mkono serikali ya Khartoum, lakini wakati huo huo isiitenge serikali ya Juba. Suda Kusini ambalo ni taifa jipya ulimwenguni, ina utajiri mkubwa wa mafuta. China ilitoa wito wa kusitishwa mapigano ya mipakani ambapo Sudan Kusini ilitwaa udhibiti wa eneo muhimu la mafuta Heglig mnamo tarehe 10 Aprili kwa siku 10.

Akiwa mjini beijing, Kiir anatarajiwa kuwasilisha hoja zake kwa mamlaka ya China, lakini wachambuzi wa siasa wanasema China haionekani kuegemea upande wowote katika suala hilo, na badala yake itaendelea kushinikiza kuwepo mazungumzo.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Hamidou Oummilkheir