1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko ya Tunisia yaua 35

11 Januari 2011

Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu, International Federation for Human Rights, limesema watu wasiopungua 35 waliuwawa kwenye maandamano ya mwishoni mwa juma

https://p.dw.com/p/zwAK
Rais wa Tunisia, Zine El Abidine Ben AliPicha: AP

Hali ya ghasia katika nchi ya Tunisia, nchi ambayo inaonekana kuwa ni tulivu, imejitokeza katika wiki kadha zilizopita. Sababu ya ghasia hizo na maandamano ni kujichoma moto kwa kijana mmoja, na jeshi la nchi hiyo kuingilia kati kwa nguvu kukandamiza maandamano yaliyofuatia. Hadi sasa mapambano makali baina ya waandamanaji na polisi yametokea mwishoni mwa juma hili. Jana Jumatatu yalitokea mapambano zaidi na rais Ben Ali ambaye yuko madarakani katika nchi hiyo kwa muda wa miaka 23 sasa, aliamuru kufungwa kwa shule na vyuo vikuu nchini humo.

Baada ya machafuko ya mwishoni mwa juma kati ya waandamanaji na polisi katikati na magharibi mwa Tunisia, serikali imesema kuwa watu 14 wameuwawa, lakini upande wa upinzani unazungumzia watu 20 waliouwawa na jana Jumatatu kumekuwa na ghasia nyingine katika eneo hilo. Jeshi la polisi lilifyatua risasi za mipira na mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji, ambapo waandamanaji walikuwa wakiwakumbuka wahanga wa machafuko ya siku zilizopita. Katika mji wa Kasserine, karibu kilometa 300 kusini mwa mji mkuu Tunis, watu walioshuhudia wamesema jeshi la polisi lilifyatua risasi za moto na watu wengi wamepigwa risasi, na ndio sababu idadi ya wahanga itakuwa ni ya juu.

Tunesien Proteste
Waandamani wakiandamana kumshinikiza rais wa Tunisia, Zine El Abidine Ben Ali, ajiuzuluPicha: AP

Kutokana na mbinyo huo wa maandamano mwishoni mwa juma kwa mara ya kwanza jeshi lilitumika. Wizara ya mambo ya ndani ya Tunisia imeeleza matumizi ya jeshi kuwa ni muhimu ili kujilinda. Kwa mwanasiasa wa upinzani Ahmed Chebbi hali hiyo ni kashfa kubwa.

Matumizi haya ya kinyama ya nguvu yanayofanywa na jeshi la usalama kabisa ni kinyume na sheria. Maandamano haya ni ya amani, watu hawana silaha na wanadai tu ajira, uhuru na heshima. Na nini serikali inachofanya? Wanawashambulia vijana. Namtaka rais, kuwataka mbwa wake hawa, waache matumizi yao ya silaha, ili Tunisia isije ikatumbukia katika hali isiyo thabiti na machafuko.

Wakati huo huo rais Zine El Abidine Ben Ali katika hotuba yake kwa njia ya televisheni amesema kuwa atatengeneza nafasi mpya 300,000 za ajira katika muda wa miaka miwili ijayo. Kwa hiyo wanafunzi wote waliomaliza masomo ya chuo kikuu watapata kazi, ambao wamekuwa hawana kazi kwa muda wa miaka miwili, watapata kazi, amesema rais huyo. Akitembelea maeneo ya ghasia rais Ben Ali amezungumzia kuhusu, magaidi, na makundi ya wahuni. Pia amezungumzia kuhusu makundi ya maadui kutoka nje, ambao wanazitumia taarifa potofu za vijana wa nchi hiyo kuleta ghasia.

Jana Jumatatu serikali imeamuru kufungwa kwa shule na vyuo vikuu nchini humo hadi zitakapotolewa taarifa zaidi, ambapo hapo kabla polisi katika eneo la kati mjini Tunis walivunja mkusanyiko wa wanafunzi wa shule na vyuo, ambapo walifanya hivyo kutokana na taarifa walizozitoa kupitia mtandao wa Intaneti.

Mwandishi Göbel, Alexander/ZR/Sekione Kitojo

Mhariri : Josephat Charo