1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko yaendelea Syria

Admin.WagnerD1 Machi 2012

Jeshi la Syria limeendelea kuushambulia mji wa Homs (29.02.2012), wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likiandaa rasimu ya azimio jipya , linaloitaka Syria kuruhusu uingizwaji wa misaada ya kibinadamu.

https://p.dw.com/p/14CK7
Mwanajeshi akiwa mjini Homs, Syria
Mwanajeshi akiwa mjini Homs, SyriaPicha: dapd

Wakati azimio hilo likiandaliwa mjini Washington, Marekani, shirika moja la haki za binadamu nchini Syria, limekana taarifa kuwa askari hao wa jeshi wameingia Baba Amr, mji ulioshambuliwa na jeshi kwa siku ya 26 mfululizo.

Mwanaharakati mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake, ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa kuwa machafuko yanaendelea pembezoni mwa mji huo, lakini vikosi hivyo havijaingia mjini humo.

Chanzo hicho cha habari kimesema, wanajeshi hao wanafanya msako wa jengo kwa jengo na nyumba kwa nyumba, wakikagua kila sehemu ili kuwakamata magaidi na silaha zao.

Hatahivyo, Shirika la kutetea haki za binadamu nchini Syria, limeripoti kuwa majeshi ya waasi yanazuia mji huo usishambuliwe.

Mwanaharakati mmoja wa mjini Homs, Hadi Abdullah, amesema ni kweli askari hao hawajaingia Baba Amr ila wameizingira wilaya hiyo, na ghasia zimeshuhudiwa maeneo ya jirani ya Inshaat na Malaab.

Abdulah amesema umeme umekatwa karibu maeneo yote ya mji huo, na kuongeza kuwa hiyo ni ishara ya kutokea kwa mashambulizi. Makamanda wa waasi nao wamesema kuwa njia zote za kuingia Homs, zimefungwa nahakuna uwezekano wa wakazi wa mji huo kupata mahitaji muhimu.

Mjini Washington, Marekani, mwanadiplomasia mmoja wa Baraza la Usalama amesema azimio hilo, linaloandaliwa sasa, linazingatia zaidi namna ya kupeleka misaada ya kibinadamu katika miji kama ya Homs, lakini azimio hilo lilitadokeza kuwa serikali ndio chanzo cha machafuko hayo.

Mataifa ya Magharibi yanatumaini kwa kutilia mkazo matatizo ya kibinadamu nchini Syria, kutaweza kuzishinikiza Urusi na China kutotumia kura zao za turufu kulipinga azimio hilo, kama zilivyofanya mwezi Oktoba, mwaka jana na mwanzoni mwa Februari.

Mjini London, Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amesema kuwa mpiga picha aliyejeruhiwa Paul Conroy amepelekwa katika ubalozi wa Uingereza mjini Beirut, Lebanon, baada ya kuondolewa mjini Homs.

Cameron amelihakikishia bunge kwamba Paul, yuko salama na amempongeza kwa ujasiri wake pamoja na wanaharakati waliomsaidia kufanikiwa kuondoka mjini humo, baada ya kushambuliwa na guruneti wakati akiwa katika kituo cha muda cha habari, ambapo mwanahabari nguli Marie Colvin na mpiga picha wa Kifaransa waliuwawa.

Kundi moja la wanaharakati wa kimataifa Avaaz, limesema wanaharakati 13 waliuwawa, wakati wakijaribu kumsaidia Paul, mwanahabari huyo wa gazeti la Sunday Times, pamoja wa waandishi wengine kuondoka nchini Syria, hapo Jumanne.

Mwandishi: Pendo Paul\ AFP

Mhariri:Abdul-Rahman