1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mada tatu kuu zimechambuliwa hii leo

Oummilkheir2 Mei 2007

Kupungua idadi ya wasiokua na ajira,uhusiano wa kiuchumi pamoja na marekani na Uturuki

https://p.dw.com/p/CHT4

Faraja katika soko la ajira nchini Ujerumani,kupimana nguvu katika uchaguzi wa rais nchini Uturuki na uhusiano wa kiuchumi kati ya Marekani na Umoja wa ulaya ni miongoni mwa mada zilizomulikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Tuanze basi na habari za kutia moyo.Kwa mara ya kwanza tangu kupita zaidi ya miaka minne,idadi ya wasiokua na kazi nchini Ujerumani imepungua katika kipindi cha mwezi wa April na kufikia chini ya watu milioni nne.Hata hivyo magazeti yanahisi hakuna sababu ya kushangiria.Na hivyo ndivyo lionavyo gazeti la RHEIN-NECKAR-ZEITUNG la mjini Heidelberg:

„Hakujakua na wakati muwafak zaidi kuliko sikukuu ya wafanyakazi,kuwaarifu wajerumani kwamba tija ya mkondo wa mageuzi imelifikia pia soko la ajira.Kwa mara ya kwanza ,idadi ya wasiokua na ajira iko chini ya watu milioni nne-na la kutia moyo zaidi ni kwamba ukuaji wa kiuchumi hautatetereka kwa kipindi kijacho.Hata hivyo kuna walakin katika ukuaji wa kiuchumi unaolinganishwa na ule wa kimarekani.Nafuu katika soko la ajira,mageuzi ya mfumo wa malipo ya watu wasiokua na ajira kwa muda mrefu,maarufu kwa jina la „ mageuzi ya Hartz“,mpango wa kuwaajiri upya watu waliopindukia miaka 50-yote hayo yanabuni nafasi za kazi lakini kwa muda tuu.Ujerumani imejiandaa kuimarisha uchumi wake.Lakini kwamba nafasi za kazi siku za mbele zitakua za milele,hapo hakuna uhakika.“

Mod: Gazeti la MÜNCHENER ABENDZEITUNG linaandika:

„Nani aliyefikiria miaka miwili iliyopita kwamba wasiokua na ajira wangefikia watu chini ya milioni nne?Wakati ule idadi yao ilipindukia milioni tano na makadirio yalikua yakitisha.Hii leo wataalam wanaashiria mema:mambo yatazidi kua mazuri.Hata hivyo hali hiyo ya kutia moyo ina ila:Licha ya ukuaji imara wa kiuchumi,bado kuna mamilioni wa watu wasiokua na ajira tangu muda mrefu sasa ambao wanashindwa kupata kazi.Waziri wa ajira anastahiki kufanya kila la kufanya kuwahui watu hao.Akifanikiwa katika uwanja huo tuu ndipo Franz Münterfering atakapoweza kujipiga kifua.”

Mada nyengine iliyoshughulikiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo inahusu uhusiano wa kiuchumi kati ya Marekani na Umoja wa ulaya.Gazeti la kiuchumi la mjini Düsseldorf-HANDELSBLATT linaandika:

“Angela Merkel anajaribu kwa kila hali kuupa umuhimu mkubwa mpango huo,kupindukia muda wa kuwepo kwake madarakani.Wanaviwanda wa Ujerumani na wale wa Marekani wanaunga mkono mpango huo.Badala yake lakini serikali ya Marekani haijajitokeza kwa moyo mkunjufu na wala haionyeshi hamu-inategea msukumo wa rais tuu.Lakini msukumo huo utatosha kweli kulitanabahisha kampuni lenye nguvu la SEC liachane na sera zake za vizuwizi.”

Mada ya mwisho magazetini hii leo inahusu uamuzi wa mahakama ya katiba ya Uturuki dhidi ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais nchini Uturuki.Kwa kufanya hivyo mahakimu wa mjini Ankara wamejifungamanisha na madai ya chama cha upinzani cha CHP.

Kuhusu mada hiyo gazeti la HAMBURGER ABENDBLATT linahisi:

„Kubatilishwa duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais ni ushahidi kwamba wanajeshi wamekua wakichochea mambo kichini chini.Lakini uamuzi huo hautositisha hata kidogo mapambano kati ya jeshi na serikali kuhusu mkondo unaobidi kufuatwa na jamii ya kituruki.Ingawa watu hawatakosea wakihoji kwamba asili mia 97 ya ardhi ya Uturuki inakutikana katika bara la Asia-hata hivyo mageuzi yaliyotiwa njiani kufumba na kufumbua na hasa na chama cha AKP yamedhihirisha, kisiasa waturuki wameingia njiani kuelekea Ulaya-ingawa njia ni ndefu na haijulikani watafika lini.“