1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madaktari wasio na mipaka kujiondoa Yemen

Admin.WagnerD19 Agosti 2016

Shirika la madaktari wasio na mipaka jana lilisema litawaondoa wafanyikazi wake kutoka hospitali linazofadhili Kaskazini mwa Yemen baada ya watu 19 kuuawa katika shambulizi la angani dhidi ya Hospitali moja.

https://p.dw.com/p/1Jlc4
Jemen Militär starte Offensive gegen Houthi-Rebellen ARCHIV
Picha: picture alliance/dpa/Str

Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya waasi nchini Yemen hii leo umesema kuwa unataka kikao cha dharura na shirika la madaktari lisilokuwa na mipaka la -MSF- kuhusiana na hatua ya kutaka kuondoa wafanyikazi wake kutoka hospitali sita katika nchi hiyo inayokumbwa na ghasia.

Hapo jana shirika hilo lenye makao yake mjini Paris liliushtumu muungano huo kwa mashambulizi ya kiholela na kusema limepoteza imani katika uwezo wa muungano huo wa kuzuia mashambulizi hatari dhidi ya hospitali hizo.

Shirika hilo lilisema kuwa watu 19 ikiwa ni pamoja na mfanyikazi wake mmoja waliuawa siku ya Jumatatu katika shambulizi la kutokea angani dhidi ya hospitali ya Abs linaloifadhili katika mkoa wa Kaskazini wa Hajjah.

Shirika hilo liliongeza kusema kuwa uamuzi wa kuondoa usaidizi wake hauchukuliwi kimzaha na kwamba kutokana na mashambulizi hayo ya kiholela, hospitali za Saada na Hajjah sio salama kwa wagonjwa na pia wafanyikazi. Shirika hilo lilisema kuwa hospitali hiyo itaendelea kusimamiwa na wafanyikazi wa eneo hilo na wale watakaojitolea.

Ärzte ohne Grenzen verlassen den Jemen
Wafanyikazi wa kimataifa wa msaada waondoka Sana'a baada ya uwanja wa ndege wa kimataifa kufunguliwa tena kwa mashirika ya msaada .Picha: picture-alliance/dpa/Y. Arhab

Hata hivyo muungano huo unaoongozwa na Saudia Arabia ulisema kuwa unathamini sana kazi inayofanywa na shirika hilo katika mazingira magumu huko Yemen.

Chanzo cha kukithiri kwa ghasia

Ghasia katika eneo la Yemen zimekithiri tangu mwezi Machi mwaka 2005 wakati waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran walipovamia na kukita mizizi katika mji wa Aden kusini mwa Yemen na kuilazimu Saudi Arabia na washirika wake wa Kisunni kuanzisha mashambulizi ya angani dhidi ya kundi hilo. Pia muungano huo uliimarisha mashambulizi yake mwezi huu baada ya mashauriano ya amani yanayoongozwa na Marekani kati ya serikali ya Yemen inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa na waasi hao kuahirishwa.

Saudia Arabia pia imeshtumiwa mara kwa mara na makundi ya kutetea haki za binadamu kuhusiana na vifo vya raia. Lakini imejitetea na kusema kuwa mara nyingi huchagua eneo linalotaka kushambulia kwanza ili kuepukana na mashambulizi ya kiholela na vifo vya raia.

Wakati huo huo, kundi la pamoja la uchunguzi linalofanya uchunguzi huru kuhusiana na mgomo katika hospitali na mashambulizi ya angani siku ya Jumamosi, dhidi ya shule ya Koranic ambayo shirika hilo limesema kuwa watoto 10 waliuawa katika mkoa wa Saada pia limetekwa nyara na waasi hao katika eneo la Kaskazini mwa Yemen.

Mwandishi: Tatu Karema

Mhariri: Josephat Charo