1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madeni ya Ulaya: Merkel agoma kulegeza msimamo

Admin.WagnerD27 Juni 2012

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amekataa shinikizo la kujumuisha deni la Ulaya kupitia hati za dhamana na kusema kuwa hatua hiyo ni hatari kabla serikali hazijaonyesha kuwa zinaweza kuheshimu sheria za bajeti.

https://p.dw.com/p/15MJU
Kansela Angela Merkel.
Kansela Angela Merkel.Picha: picture alliance/dpa

Merkel ameweka msimamo huo siku moja kabla ya mkutano Mkuu wa mataifa yanayotumia sarafu ya euro unaolenga kutafuta njia za kunusuru uchumi wa kanda hiyo. Merkel ambaye yuko safarini kuelekea ufaransa kukutana na rais wa nchini hiyo Francois Hollande, amesema kujumuisha madeni ya Ulaya ni njia isiyo sahihi na kunaweza kusababisha kurudiwa kwa makosa yaliyofanyika huko nyuma.

Shinikizo linazidi kuongezeka kwa Kansela huyo kulegeza msimamo wake juu ya utoaji wa dhamana za pamoja wakati ambapo Hispania nayo inaonyesha dalili za kutaka kuokolewa.

Noti za euro.
Noti za euro.Picha: picture-alliance/dpa

Masharti ya dhamana
Alisema dhamana na udhibiti laazima viende sambamba na kwamba kunaweza kuwa na dhima ya pamoja pale tu udhitibi wa kutosha utakapowekwa. Licha ya ukweli kwamba mifumo kama hati na bili za ulaya, na ukombozi wa madeni vinakwenda kinyume na katiba ya Ujerumani, Merkel alisema yeye mwenyewe anavichukulia kama njia isiyo sahihi na ya hatari.

Wataalamu wanasema ingawa hati hizi za dhamana za ulaya zinaweza kupunguza gharama za ukopaji kwa mataifa yanayohangaika na mzigo wa madeni kama Hispania na Italia, zinaweza kupandisha gharama hizi kwa Ujerumani na baadhi ya nchi nyingine ambazo hazijaathirika sana. Utawala mjini Berlin una hofia kubeba madeni ya mataifa mengine bila kuwa na uhakika kwamba mataifa hayo yanachukua hatua za kufanya mageuzi ya kiuchumi.

Katika maandalizi ya Mkutano huu muhimu kwa hatma ya kanda ya euro, maafisa wa juu wa Umoja wa Ulaya wametayarisha mpango wenye mapendekezo ya muda wa kati kuelekea dhamana za ulaya, pamoja na uanzishwaji wa muungano wa mabenki chini ya mamlaka moja. Wametaka pia mataifa 17 wanachama wa kanda hiyo kusalimisha udhibiti zaidi wa bajeti zao katika kile kinachoonekana kama kukubaliana na matakwa ya Ujerumani.

Waziri Mkuu wa Hispania, Mariano Rajoy ambaye amepiga kengele ya hatari.
Waziri Mkuu wa Hispania, Mariano Rajoy ambaye amepiga kengele ya hatari.Picha: AP

Mpango mpya kujumlisha ukuzaji uchumi
Sual muhimu katika Mkutano huo wa Mjini Brussels linatarajiwa kuwa kurekebisha mpango wa sasa wa kubana matumizi na kuongeza kipengele cha ukuzaji wa uchumi ambacho kitaongeza kiasi cha euro bilioni 130 lakini viongozi pia watahitaji kujadili mustakabali wa kanda hii inayokabiliwa kwa muongo unaokuja, ikiwa ni pamoja na kutaka ushirikiano zaidi na kuanzisha muungano wa mabenki na kukabidhi mamlaka juu ya sekta za fedha na bajeti kwa ngazi ya Ulaya.

Merkel alisema hakuna njia rahisi au ya kimuujiza ya kutatua mogogoro wa uchumi wa kanda ya euro na kutahadharisha juu ya kuwa na matumaini yaliyopitiliza katika uwezo wa nchi yake. Wakati huo huo viongozi wa Ulaya wamepata onyo lingine baada ya Waziri Mkuu wa Hispania, ambayo inakabiliwa na mgogoro wa kiuchumi, Mariano Rajoy kusema kuwa nchi yake haiwezi tena kujiendesha kutokana na viwango vikubwa inavyolipa katika masoko.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE\APE
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman