1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MADRID : Rais wa zamani wa Argentina akamatwa na kuachiliwa

13 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCb9

Rais wa zamani wa Argentina Isabel Peron ameachiliwa huru hapo jana baada ya kukamatwa nchini Uhispania chini ya hati ya kimataifa inayotaka akabiliane na mashtaka nchini mwake kuhusiana na uhalifu uliotendeka wakati wa utawala wake.

Hakimu katika mahkama kuu ya Jinai nchini Uhispania Juan el Olmo ameamuru kiongozi huyo wa zamani wa kike ambaye anagoma kurudishwa nchini mwake aachiliwe kwa masharti na afikishwe tena mahkamaní katika kipindi cha wiki mbili.

Hakimu wa Argentina ameamuru kukamatwa kwake kujibu mashtaka ya kutoweka kwa wanaharakati wa sera za mrengo wa shoto katika miaka ya 1970.Peron pia anachunguzwa na hakimu mwengine nchini Argentina kuhusiana na uhusiano wake na vikosi vya mauaji vya sera za mrengo wa kulia ambavyo inadaiwa kuwa vimeuwa watu 1,500.

Peron mwenye umri wa miaka 75 ni mjane wa aliekuwa Rais wa Argentina mara tatu Juan Peron na yeye mwenyewe aliapishwa kuwa rais hapo mwaka 1974 kufuatia kifo cha mume wake.

Serikali yake ilipinduliwa hapo mwaka 1976 na amekuwa akiishi nchini Uhispania tokea mwaka 1981 ambapo amekuwa haonekani hadharani kabisa,anakwepa macho ya udadisi ya majirani zake na kukataa maombi yote ya kufanyiwa mahojiano.