1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelefu waandamana Bangui kupinga vikosi ya usalama

23 Desemba 2013

Maelfu ya waandamanaji wameendelea kuandamana mjini Bangui, huku vikosi vya Usalama vya Umoja wa Afrika vikiripotiwa kuwafyatulia risasi, na kusababisha kifo na kujeruhiwa.

https://p.dw.com/p/1Af4D
Waandamanaji wapinga vikosi vya usalama.
Waandamanaji wapinga vikosi vya usalama.Picha: picture-alliance/AP

Waandamanaji hao walikusanyika katika geti la kuingilia uwanja wa ndege katika mji mkuu, Bangui, wakishinikiza kuondoka madarakani kwa rais wa serikali ya mpito inayoongozwa na Michel Djotodia, pia wakipinga kuendelea kuwepo kwa vikosi vya kulinda usalama vya Umoja wa Afrika.

Waandamanaji hao wa kikristu wanashinikiza kuondolewa kwa vikosi vya usalama kutoka Chad na kuwaacha askari wa Kifaransa, ambao wamekuwa wakifanya juhudi za kurejesha amani nchini humo.

Wanapinga utawala wa rais Michel Djotodia, rais wa kwanza wa kiislamu kuongoza taifa hilo, lenye idadi kubwa ya wakristu na hivyo kusababisha kuendelea kwa mapigano baina ya raia na waasi.

Wakati magari mawili ya vikosi vya usalama vya Umoja wa Afrika kutoka Chad yaliposogea karibu na eneo la waandamanaji hao hii leo , muda mfupi baadaye waandamanaji hao walianza kurusha mawe upande yalipoelekea magari hayo ndipo wanajeshi hao walipofyatua risasi za kutuliza ghasia na kujeruhi watu kadhaa na mtu mmoja kuuawa.

Askari wa Kifaransa watuliza ghasia

Hata hivyo vikosi vya usalama kutoka Ufaransa viliingilia kati kuzima ghasia hizo na kuanza kuwaokoa majeruhi.

Mmoja auwa na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Mmoja auwa na wengine kadhaa kujeruhiwa.Picha: 2013 Marcus Bleasdale/VII for Human Rights Watch

Pia maelfu wa waandamanaji wa kiislamu wanaounga mkono kundi la waasi la Seleka waliandamana jana katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui.

Waandamanaji hao walipiga kelele wakidai kuwa rais Francois Hollande wa Ufaransa ni mtuhumiwa na kuvilalamikia vikosi vyake vya kulinda usalama kuwa vinaegemea zaidi kuwalinda wakristu.

Raia wengi wa Bangui wanailaumu Chad ambayo rais wake Idriss Deby Itno amekuwa anacheza karata ya nani aongoze Jamhuri ya Afrika ya kati na muasisi wa kikundi cha waasi cha Seleka.

Chad ni sehemu ya vikosi vya uslama vya kulinda amani Jamhuri ya Afrika ya kati ya wanajeshi 3,700 kutoka vikosi kutoka nchi za Afrika wanaolinda usalama.

Jumuiya za kimataifa zaonya

Jamahuri ya Afrika ya kati inakabiliwa na miezi ya mapigano, vitendo vya ubakaji na vurugu mbali mbali, jambo ambalo jumuiya za kimataifa zimetoa onyo juu ya kuendelea kuvunjika kwa haki za binaanadamu dhidi ya raia.

Mbali ya Ufaransa kupeleka askari 1,600 wa Kifaransa chini ya idhini ya Umoja wa Mataifa mapema mwezi huu kulisaidia kurejesha amani kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui, ingawaje bado mashambulizi ya kulipiziana kisasi yanaendelea.

Askari wa Kifaransa wanaungwa mkono na wakristu huku wakionekana kutofautiana na wasilamu wanaounga mkono waasi wa selekea, ambao maelefu waliandamana jana mjini Bangui kuwapinga askari hao na kusababisha mapigano yaliyopelekea kuuawa kwa waasi watatu wa kundi la Seleka.

Askari wa Kifaransa wapingwa na waislamu wanaounga mkono waasi wa Seleka.
Askari wa Kifaransa wapingwa na waislamu wanaounga mkono waasi wa Seleka.Picha: picture-alliance/AP

Djotodia, aliwekwa kama rais wa muda chini ya mkataba maalumu ulioafikiwa na mataifa ya Afrika lakini kwa sasa anaonekana kuzidiwa nguvu na kushindwa kwake kuzuia umwagikaji damu ambao unaendelea.

Mwandishi: Flora Nzema/AFP

Mhariri: Saumu Yusuph Mwasimba