1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano Barcelona kuunga mkono kura ya Catalonia

Sylvia Mwehozi
20 Septemba 2017

Maelfu ya waandamanaji wenye hasira wameingia katika mitaa ya mji wa Barcelona, baada ya polisi wa Uhispania kuwakamata jumla ya viongozi 13 wa Catalonia kuelekea katika kura ya maoni.

https://p.dw.com/p/2kOJT
Spanien Proteste nach der Festanahme von Josep Maria Jove in Barcelona
Picha: Reuters/A. Gea

Wakati mvutano ukizidi kuongezeka makundi ya wale wanaotaka kujitenga yamehimiza watu zaidi kuandamana kupinga kukandamizwa kwa viongozi katika mkoa huo wa kaskazini mashariki, wakati maandalizi ya kura hiyo itakayofanyika Oktoba Mosi yakiendelea, licha ya zuio la kutoka serikali kuu ya Uhispania na uamuzi wa mahakama wa kusema ni kinyume na katiba.

Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy ametoa wito wa utulivu akidai kwamba "hali itarejea kuwa ya kawaida kwa sababu kura hiyo ya maoni haiwezi kufanyika." Lakini Rais Carles Puigdemont wa Catalonia ameishutumu serikali ya Rajoy kwa kutangaza hali ya hatari na kwa kujaribu kuizuia kura hiyo.

Spanien - Unabhängigkeitsreferendum für Katalonien - Mariano Rajoy
Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano RajoyPicha: Reuters/S. Vera

Msemaji wa serikali ya mkoa huo amesema miongoni mwa waliokamatwa na polisi ni Joseph Maria Jove, katibu mkuu wa masuala ya kiuchumi na makamu wa rais wa Catalonia, pamoja na maafisa wengine wanaofanya kazi katika idara mbalimbali za serikali ya Catalonia. Sababu ya kukamatwa kwao haikuwekwa wazi, lakini serikali kuu ya Uhispania imeonya kwamba mafisa wanaosaidia kuratibu kura ya maoni watakabiliwa na mashitaka. Polisi wanasema wamejipanga kwa ajili ya operesheni 22 za ukaguzi.

Katikati mwa Barcelona kwenyewe, maelfu ya waandamanaji walikusanyika karibu na ofisi ya Jovi, wengi wakionekana katika rangi za bendera ya Catalonia nyekundu na njano, wakiimba"uhuru"! na "tutapiga kura". Shirika moja lenye ushawishi na linalounga mkono uhuru wa Catalonia la Catalan Nationa Assembly, ANC, limewataka wananchi wa Catalonia kujiunga na maandamano hayo.

Operesheni za polisi zinakuja siku moja baada ya maafisa kukamata nyaraka zinazohusiana na kura hiyo ya kujipatia uhuru kutoka katika ofisi ya Unipost, kampuni binafsi ya usafirishaji mjini Terrassa karibu na Barcelona. Polisi wanasema wanashikilia nyaraka za taarifa 45,000 zilizokuwa zitumwe kwa Wacatalonia waliochaguliwa kusimamia kura hiyo katika vituo vya kupigia kura ikiwakilisha asilimia 80 ya idadi inayotakiwa kuhakikisha vituo vilikuwa na wafanyakazi wa kutosha.

Spanien - Unabhängigkeitsreferendum für Katalonien
Rais wa serikali ya mkoa wa catalonia Carles PuigdemontPicha: picture-alliance/Zumapress.com/J. Boixareu

Polisi pia waliwafunga waandamanaji kadhaa ambao walikusanyika nje ya ofisi ya Unipost ili kuzuia maafisa wa polisi kuingia ndani ya jengo hilo. Madrid imetishia kuwakamata mameya wanaoratibu kura hiyo. Mvutano pia umefika hadi bungeni mjini Madrid ambako mbunge wa chama cha mrengo wa kushoto cha wale wanaotaka kujitenga amemueleza waziri mkuu Rajoy kuwa "aondoe mikono yake michafu katika taasisi za Catalonia."

Utafiti wa maoni unaonyesha kwamba Catalonia iliyo na karibu wakazi milini 7.5 imegawanyika kuhusu suala la kujitenga kutoka Uhispania na kujipatia uhuru. Utafiti wa mwezi Julai ulisema kwamba asilimia 49.5 ya Wacatalonia wanapinga suala hilo wakati aislimia 41 wanaunga mkono ingawa asilimia 70 wanasema wanataka kura ya maoni ili kumaliza suala hilo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/afp

Mhariri: Mohammed Khelef