1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waandamana Marekani kupinga amri ya Trump

Sylvia Mwehozi
30 Januari 2017

Amri iliyojaa utata iliyotolewa na Rais Donald Trump ya kupiga marufuku wasafiri kutoka nchi saba za kiislamu kuingia nchini Marekani imeibua hasira na maandamano makubwa  nchini humo.

https://p.dw.com/p/2WcDV
US-Einreiseverbot gegen Muslime: Widerstand in den USA
Picha: Picture-Alliance/AP Photo/K. Willens

Marufuku hiyo imekosolewa na washirika wake na kuleta mkanganyiko juu ya utekelezaji wake miongoni mwa WaRepublican na wademocratic ambao wanatafuta fimbo ya kumuadhibu Trump.

Majaji wanne wa shirikisho walifikia hatua ya kuingilia kati kusimamisha zuio hilo, huku kiasi ya watu karibu 300 wakizuiliwa au kusimamishwa duniani kote kuingia Marekani na wanasheria wa haki za kiraia nchini humo wameonya kuwa kuna uwezekano wa kuibuka kwa mvutano baina ya uongozi wa Trump na Mahakama kuu.

USA Amerika protestiert gegen den Einreiseverbot für Muslime
Mwanamke muandamanaji akiwa amevalia Hijab yenye bendera ya MarekaniPicha: Reuters/S. Keith

Amri hiyo ilizuia kuwasili kwa wakimbizi wote kwa karibu siku 120 huku kutoka Syria ikiwa ni marufuku isiyo na kikomo na wengine kutoka Iran, Iraq, Libya, Somalia, Sudan, Syria na Yemen wakizuiliwa kwa muda wa siku 90.

Maelfu ya waandamanaji walikusanyika katika mitaa ya majiji mbalimbali nchini humo na katika viwanja vya ndege mwishoni mwa juma kupinga amri hiyo wakati wanasheria walipofanya jitihada za kuwaachiliwa kwa wale waliozuiliwa baada ya kuwasili katika viwanja vya ndege. Kauli ya Donald Trump aliyoitoa imesisitiza kuwa katu hiyo sio marufuku dhidi ya waislamu."Kabisa hii sio marufuku dhidi ya waislamu lakini tumejiandaa na inafanya kazi vyema. Unaona katika viwanja vya ndege! unaona inavyofanya kazi, ni suala linalokwenda vyema. Na tutakuwa na marufuku kali na kufanya maamuzi ambayo tulipaswa kuyafanya katika nchi hii kwa miaka mingi, " amesema Trump.

Jijini New York inakadiriwa kuwa waandamanaji elfu 10 walikusanyika katika viwanja vya wazi vya Battery karibu na mnara wa uhuru huku wengine kadhaa wakiandamana nje ya Ikulu ya white House. Mamia  pia waliandamana huko Boston, Washington na katika miji mengine kadhaa. 

USA Tausende demonstrieren an US-Flughäfen gegen Trumps Einreisebann
Waandamanaji katika uwanja wa ndege wa John F. Kennedy jijini New YorkPicha: picture alliance/AP Photo/C. Ruttle

Mmoja wa waandamanaji jijini New York anasema, "Mimi ni mhamiaji. Nimeishi New York kwa miaka 10 na hii ni moja ya jambo baya lililowahi kutokea. Namaanisha kuweka mtihani wa udini katika nchi hii sijawahi sikia na nafikiri ni wakati wa kila mmoja kusimama na nimekuja na watoto hapa, mke wangu melissa na watoto wangu wawili ili kuonyesha kwamba tunasimama kwa ajili ya jambo lililo sahihi."

Viongozi mbalimbali ulimwenguni wamelaani hatua hiyo, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amemueleza Trump kuwa vita vya kimataifa dhidi ya ugaidi sio sababu ya kuwazuia wakimbizi au watu kutoka nchi za Kiislamu kuingia nchini Marekani.

Yemen ambayo ni moja ya nchi iliyomo katika marufuku hiyo imeonya kuwa amri hiyo itachochea ugaidi zaidi duniani kote, ikisema haijaridhishwa na zuio lililowekwa dhidi ya raia wake kuingia Marekani.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/Reuters

Mhariri: Saumu Yusuf