1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wafurika katika kambi za UNAMID, Darfur

8 Aprili 2013

Maelfu ya raia katika jimbo linalokumbwa na machafuko la Darfur nchini Sudan wametafuta hifadhi karibu na kambi za majeshi ya kulinda amani baada ya kutokea mashambulizi ya waasi

https://p.dw.com/p/18BWw
epa02486116 A handout photograph made avialable by the United Nations Assistance Mission in Darfur (UNAMID) on 08 December 2010 shows some of the residents of Kalma camp, for internally displaced persons (IDPs). in Nyala, South Darfur, with their belongings before begining to return to their homes of bild-epa in West Darfur on 07 December 2010. Reports state that the exercise is expected to conclude on 12 December 2010. This is the first government owned operation with the assistance of UN Agencies in the area.The IDPs will return to Tandusa, Andi, Gido, Sullu and Urum villages in West Darfur located about 90 and 150 kilometers south of El Geneina town. United Nations High Commission for Refugees (UNHCR) and Office for the Coordination of Humanitarian Affairs (OCHA) distributed non food items including blankets, jerricans and sleeping mats to each household to use on the journey. EPA/ALBERT GONZALEZ FARRAN / UNAMID / HANDOUT EDITORIAL USE ONLY/NO SALES +++(c) dpa - Bildfunk+++
Kalma CampPicha: picture-alliance/dpa

Hayo yanajiri wakati wahisani wa kimataifa wakitafuta fedha za kulisaidia eneo hilo lililoharibiwa na mgogoro uliodumu muongo mmoja sasa. Nchini Sudan kwenyewe waasi wamelishutumu vikali kongamano hilo linalokamilika hii leo mjini Doha, Qatar. Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa, UNAMID, katika jimbo la Darfur, umethibitisha jana Jumapili kuwa waasi wa kundi la Minni Minnawi la Sudan Liberation Army wameishambulia na kuitwaa miji ya Muhagiriya na Labado. Pia kumekuwa na ripoti za uwezekano wa mashambulizi yaliyofanywa kutokea angani.

Taarifa ya jeshi la UNAMID inasema maelfu ya raia wengi wao wakiwa na mifugo yao, wamejazana katika kambi za UNAMID na shinikizo kutokana na idadi kubwa ya wakaazi linaongezeka. Siku ya Jumamosi, waasi walisema waliwauwa wanajeshi wa serikali na kuyadhibiti maeneo hayo mashariki ya mji wa kusini mwa Darfur wa Nyala.

Hamad bin Jassim bin Jabr Al-Thani akizunguamza katika kongamano la wahisani Doha
Waziri Mkuu Hamad bin Jassim bin Jabr Al-Thani akizungumza katika kongamano la wahisani DohaPicha: Reuters

Vurugu hizo za karibuni, zimekuja wakati wanamgambo ambao wamekuwa wakipigana kwa miaka 10 katika jimbo la Darfur, wakilishutumu kongamano la kimataifa la wahisani mjini Doha, Qatar, ambalo linatafuta msaada wa kulijenga upya eneo lililoharibiwa na vita la Darfur.

Abdel Wahid Mohammed al-Nur ambaye anaongoza kundi jingine la Sudan Liberation Army - SLA, amesema kwa kuandaa mkutano wa wahisani, ni lazima kwanza pawepo amani na usalama. Gibril Adam Bilal, msemaji wa kundi a Justice and Equality Movement – JEM ameitaka jamii ya kimataifa kutoipa serikali ya Sudan nafasi ya kufanya uhalifu dhidi ya binaadamu.

Kongamano hilo la Doha ambalo linakamilika leo, lilikubaliwa chini ya mpango wa amani wa Julai 2011 ambao Khartoum iliusaini katika mji huo mkuu wa Qatar, pamoja na makundi yaliyojigawanya ya waasi.

Waasi wa SLA na JEM wanakataa kusaini mpango wa amani uliofikiwa mjini Doha Julai mwaka 2011
Waasi wa SLA na JEM wanakataa kusaini mpango wa amani uliofikiwa mjini Doha Julai mwaka 2011Picha: Reuters

Katika hotuba yake, makamu wa rais wa Sudan Ali Osman Taha ameyataka makundi yote yenye silaha kufanya uamuzi wa kihistoria wa kuheshimu matumaini ya watu wa Darfur, akimaanisha waasi ambao kufikia sasa wamekataa kujiunga na makubaliano ya amani ya mwaka wa 2011. Makundi makuu ya waasi ikiwa ni pamoja na JEM na SLA yamekataa kusaini mkataba huo, ijapokuwa kundi moja lililojitenga na JEM lilisaini mpango huo katika mkesha wa kongamano la Doha.

Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Hamad bin Jassem Al-Thani amesema wakati wa amani ambayo italindwa na maendeleo na wala siyo matumizi ya nguvu, umeanza Darfur. Mkutano huo unanuia kuweka mkakati wa maendeleo unaohitaji euro bilioni 5.5 kwa juhudi za miaka sita kuondoa Darfur kutoka matatizo ya kupewa misaada ya chakula na misaada mingine ya dharura, na kuweka misingi imara ya miradi ya maji, barabara na miundo mbinu.

Uingereza imeahidi msaada wa karibu euro milioni 13 kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kusaidia jamii katika jimbo la Darfur kupanda vyakula vyao na kutoa mafunzo ya ujuzi kuwasaidia watu kupata kazi. Jana Jumapili, watu waliowachwa bila makaazi wamefanya maandamano katika kambi kadhaa za Darfur wakitaka usalama upewe kipau mbele, huku wengine wakisema hawatarudi katika vijiji vyao hadi pale amani itakaporejeshwa.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef