1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waikimbia mionzi ya nyuklia Japan

16 Machi 2011

Maelfu ya watu hivi wanakimbia nchini Japan kwa lengo la kunusuru maisha yao kufuatia balaa la kuvuja kwa mionzi ya nyuklia baada kuripuka kwa vinu vya nyuklia huko Fukushima Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/10ZoY
Athari za tetemeko la ardhi na tsunami nchini Japan
Athari za tetemeko la ardhi na tsunami nchini JapanPicha: dapd

Wakati mwingine msiba unakua neema kwa wauza majeneza,katika suala kukimbia Japan mashirika madogo madogo ya ndege yamekuwa yakineemekea kwa hivi sasa kwa kupata idadi kubwa ya abiria kuliko kawaida.

Tathmini ya sasa inaonesha kuwa mahitaji ya kubeba abiria kwa wasafirishaji hao imeongezeka huku bei ya safari nayo ikiwa imepandishwa.

Lakini pamoja na wasafiri binafsi, makampuni ya kimataifa nchini Japan wamekuwa wateja wakubwa wanaosafirisha wafanyakazi wao waliopo katika jiji la Tokyo pamoja na maeneo ya karibu kutokana na kitisho cha mionzi.

Waokoaji wakitafuta miili ya walofariki kutokana na tetemeko na tsunami
Waokoaji wakitafuta miili ya walofariki kutokana na tetemeko na tsunamiPicha: AP

Wengi wa wasafiri hao wanakimbilia katika maeneo ya Hong Kong, Taiwan, Korea Kusini, Australia pamoja na Marekani katika kipindi hiki ambacho ambacho hata baadhi ya viwanda vimesitisha uzalishaji kutokana zahama ya tetemeko na tsunami iliyotokea ijumaa iliyopita.

Msafirishi mmoja wa kampuni ya binafsi ya ndege ya China Jackie Wu amenukuliwa akisema amepata kazi ya kusafirisha abiria 14 kutoka Tokyo na kuongeza kuwa abiria hao kwa sasa hawajali kabisa kuhusu kiwango cha nauli ambacho kimeongezeka mara dufu.

Msafirishaji mwingine, Mike Walsh, amesema mahitaji ya wateja waliyopo Tokyo na hasa wanaotaka kwenda Hong Kong inazidi uwezo wao wa kusafirisha.

Mike, ambae ni mkuu wa kampuni binafsi ya ndege katika maeneo ya bara la Asia, amesema kwa leo hii (16-03-2011) pekee wanashughulika na abiria zaidi ya 1000 wanaotaka kuokolewa kutoka Tokyo.

Mapema leo mfalme wa Akihito wa Japan amejitokeza hadharani na kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari lakini safari hii alionesha dhahiri kama maji basi yamefika yamefika shingoni.

Mfalme huyo, akiwa na sura yenye majonzi, amesema yupo katika ibada ya kuwaombea manusura wa tetemeko na tsunami pamoja na zahama ya kuvuja kwa nyuklia.

Mfalme Akihito, mwenye umri wa miaka 77, amekiri kwamba mkasa huu wa sasa ni mkubwa na kwamba mpaka sasa Japan haijui idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na tukio hilo la Machi 11.

Kazi ya uokaji inaendelea ambapo, pamoja na mambo mengine, inachagizwa na uhaba wa umeme huku kitisho cha mionzi ya nyuklia iliyosambaa hewani.

Idadi ya wanaokisiwa kupoteza maisha kutokana balaa hilo mpaka sasa ni 11,000 ambapo watu 3,676 wamethibitishwa kufariki dunia.

Mwandishi: Sudi Mnette AFP/RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman