1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wakimbia mapigano mjini Juba

10 Julai 2016

Mapigano makali yamezuka Jumapili (10.07.2016) katika mji mkuu wa Sudan Kusini wa Juba na kupelekea maelfu ya watu kuukimbia mji huo kufuatia siku kadhaa za mapambano kati ya vikosi vya serikali na waasi

https://p.dw.com/p/1JMbj
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Patinkin

Mapigano makali yamezuka Jumapili (10.07.2016) katika mji mkuu wa Sudan Kusini wa Juba na kupelekea maelfu ya watu kuukimbia mji huo kufuatia siku kadhaa za mapambano kati ya vikosi vya serikali na waasi.

Mashuhuda wamesema sehemu kubwa ya mapigano hayo yametokea katika kitongoji cha Jebel ambapo makamo wa rais Riek Machar kiongozi wa waasi hadi hapo ilipoundwa serikali ya umoja wa kitaifa alikuwa na makaazi yake.

Msemaji wa kiongozi huyo James Gatdet amesema vikosi vya Rais Silva Kiir vilishambulia sehemu za Machar huko Jebel.Gatdet ameandika katika ukurasa wa Facebook kwamba vikosi vyao vimeteka vifaru vitatu kutoka vikosi vya Kiir vilioshambulia Jebel. Ameongeza kusema kwamba shambulio lao hilo limezimwa na kwamba mashambulizi yao kwa kutumia helikopta hivi sasa yamesitishwa baada ya moja ya helikopta hizo nusura iangushwe.

Hali katika mji huo bado ni tete na kuna mapambano katika baadhi ya maeneo ya mji huo.Radio Tamazuj ya ndani ya nchi imetangaza kwamba makombora yaliyofyetuliwa kwa mizinga yameangukia katika kambi ya Umoja wa Mataifa karibu na Jebel ambapo watu wengi wamejeruhiwa wakiwemo wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na watu waliopotezewa makaazi yao.

Mfanyakazi wa misaada aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina anakadiria kwamba watu 10,000 wameukimbia mji huo.Gregor Fischer mpiga picha wa Ujerumani amesema kulikuwa na mashambuliano makubwa ya risasi wakati wa asubuhi na kwamba wamekuwa wakisikia milio ya risasi,mizinga na helikopta zikiruka.Pia ameshuhudia vifaru vya serikali katika mji huo.

Idadi ya vifo ni 270

Maafisa katika ofisi ya rais wamesema idadi ya vifo imefikia watu 270 tokea kuzuka kwa mapigano hayo hapo Ijumaa na kwamba kuna majeruhi 210 kwa upande wa Machar na 60 kwa upande wa Kiir.

Waandishi wa habari wakijibanza kufuatia milio ya risasi kabla ya mkutanao wa Ras Salva Kiir na makamo wake Riek Machar mjini Juba.
Waandishi wa habari wakijibanza kufuatia milio ya risasi kabla ya mkutanao wa Ras Salva Kiir na makamo wake Riek Machar mjini Juba.Picha: picture alliance/dpa

Raia wamekuwa wakikimbilia katika maeneo mawili ya Umoja wa Mataifa na mashahidi wanasema maelfu ya watu wengine wamekuwa pia wakikimbia kutoka Juba kuelekea Gurei kama kilomita 20 magharibi mwa mji mkuu.

Hapo awali ubalozi wa Marekani uliripoti kutokea kwa mapigano katika mji wote wa Juba ukiwemo uwanja wa ndege.Kutokana na wasi wasi wa hali ya usalama katika mji huo shirika la ndege la Kenya limetangaza kusitisha safari zake katika mji mkuu huo.

Pigo kwa amani

Machafuko hayo yamekuwa yakiendelea tokea Alhamisi wakati mapambano yalipozuka kati ya vikosi vya serikali na waasi.Hapo Ijumaa mapigano yalizuka karibu na kasri la rais ambapo Kiir alikuwa akikutana na Machar.

Mwanjeshi wa kundi la Machar mjini Juba.
Mwanjeshi wa kundi la Machar mjini Juba.Picha: picture-alliance/dpa/A. M. Kerber

Kuibuka kwa mapigano hayo kumekuwa pigo kwa matumaini ya amani baada ya makundi hayo yanayohasimiana kuunda serikali ya umoja wa kitaifa hapo mwezi wa Aprili wakati nchi hiyo ikiwa ndio kwanza imeadhimisha miaka mitano ya uhuru wake kutoka Sudan hapo Jumamosi.

Mapambano ya kuwania madaraka kati ya Kiir na Machar ambayo yaligeuka kuwa mapamano ya kijeshi hapo mwezi wa Disemba mwaka 2013 yameuwa maelfu ya watu na kuwapotezea makaazi watu milioni mbili.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa/Reuters

Mhariri : Sylvia Mwehozi