1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wangojea misaada Pakistan

3 Agosti 2010

Zaidi ya watu 1,400 wamepoteza maisha yao na wengine zaidi ya milioni 3 wamethirika vibaya na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa za msimu wa masika, katika kaskazini-magharibi ya Pakistan.

https://p.dw.com/p/Oapu
A Pakistan army helicopter evacuates stranded villagers in Nowshera, Pakistan on Friday, July 30, 2010. Boats and helicopters struggled to reach hundreds of thousands of villagers cut off by floods in northwest Pakistan on Friday as the government said it was the deadliest such disaster to hit the region since 1929. (AP Photo/Mohammad Sajjad)
Helikopta ya jeshi ikiokoa watu walionasa katika kijiji cha Nowshera,Pakistan.Picha: ap

Serikali ya Pakistan inajitahidi kuwasaidia wahanga ambao wengi wao wamepoteza kila kitu. Helikopta ndio njia pekee ya kuwafikia wahanga hao walionasa katika vijiji vilivyozingirwa na maji. Wanajeshi pia wamepelekwa kusaidia, lakini hawatoshi kuhudumia umati wa watu unaongojea misaada ya dharura na wengi wao wanalalamika kuwa serikali wala haijali kama alivzosikitika mama mmoja.

" Mpaka sasa hakuna waziri ye yote yule aliekuja kujua hali zetu. Wanajeshi ndio wanaotusaidia."

Mama huyo si peke yake kulalamika kuhusu wanasiasa wao na kuwa hatua za kuwaokoa na kuwapatia misaada zinakawia. Sasa pia kuna hofu kuwa wanamgambo huenda wakaingilia kati, katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Kaskazini-Magharibi.

Mashirika ya misaada kama vile shirika la Umoja wa Mataifa WFP, linaloshughulikia mipango ya chakula duniani, yanajitahidi yawezavyo, kupunguza dhiki za wahanga hao wa mafuriko. Mwenyekiti wa tawi la WFP katika kanda hiyo,Dominique Frankefort anasema kuwa hadi sasa, wameweza kuokoa kama familia 6,000 na juma hili, wanatazamia kusadia familia zingine 35,000. Bado kuna maelfu na maelfu ya watu walionasa katika maeneo ambayo ni shida kufikisha misaada. Wale waliookolewa, wanaishi katika kambi za wakimbizi na wala hawajui jinsi maisha yao yatakavyokuwa katika siku zijazo.

Wakati huo huo, misaada ya kimataifa inamiminika nchini Pakistan. Umoja wa Ulaya, Marekani na Umoja wa Mataifa zimeahaidi mamilioni na mashirika ya misaada yametoa mwito kwa wafadhili kutoa michango zaidi. Vile vile, kuna hatari kubwa ya magonjwa ya kuambukizana kuripuka. Ama hakuna kabisa maji ya kunywa au yaliyokuwepo ni machafu.

Kama mchambuzi mmoja alivyoeleza: hivi sasa, Pakistan haikabiliwi tu na maadui Taliban bali inapambana na maafa ya kimaumbile vile vile. Mara nyingine tena kumezuka suala iwapo Rais wa Pakistan Asif Ali Zardari kweli amejizatiti na ana uwezo wa kutenzua matatizo yanayoikabili nchi hiyo na iwapo hatimae ataweza kuleta hali ya utulivu nchini humo.

Mwandishi:Küstner,Kai/ZPR/P.Martin

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman