1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Mafanikio makubwa yaripotiwa katika vita vya Gaza

Tatu Karema
4 Machi 2024

Wapatanishi katika mzozo kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Hamas katika Ukanda wa Gaza pamoja na wajumbe wa Hamas, wamepata mafanikio makubwa kuelekea usitishaji wa vita kwenye ukanda huo

https://p.dw.com/p/4d8LJ
Raia wa Palestina wanaangalia uharibifu uliosababishwa na shambulizi la Israel katika mji wa Rafah katika ukanda wa Gaza mnamo Machi 3,2024
Jengo laporomoka kutokana na shambulizi la Israel katika ukanda wa GazaPicha: Hatem Ali/AP Photo/picture alliance

Al-Qahera, inayohusishwa na idara za kijasusi za Misri, ilimnukuu afisa mmoja mkuu ambaye hakutajwa jina akisema, Misri inaendelea na juhudi zake za kufikia mapatano kabla ya mwezi mtukufu wa Ramadhani unaoanza Machi 10 au 11.

Ripoti ya kituo hicho imesema kumekuwa na maendeleo makubwa katika mazungumzo hayo bila ya uwakilishi waIsrael.

Israel haikutuma ujumbe wake katika mazungumzo

Israel haikutuma ujumbe wake katika mazungumzo hayo ya hivi  karibuni mjini Cairo yanayolenga kufikia usitishaji mapigano katika Ukanda wa Gaza na kubadilishana mateka wanaoshikiliwa na wapiganaji katika eneo hilo na wafungwa wa Kipalestina nchini Israel.

Soma pia:Dunia yalaani shambulizi la Israel dhidi ya Wapalestina Gaza

Israel inataka orodha ya mateka ambao bado wanashikiliwa na Hamas kabla ya kukubali kushiriki katika mazungumzo ambayo Marekani, Misri na Qatar zimekuwa zikijaribu kuyasimamia kwa wiki kadhaa sasa.

Maafisa wa Israel wanasema pia wanataka ufafanuzi kuhusu idadi ya wafungwa ambao kundi la Hamas linataka kuachiliwa kwa kila mateka atakayeachiwa huru.

Benny Gantz afanya ziara nchini Marekani

Gantz, mpinzani mkuu wa kisiasa wa Netanyahu, anatarajiwa kukutana wiki hii na maafisa kadhaa wakuu wa serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani ikiwa ni pamoja na Makamu wa Rais Kamala Harris, waziri wa mambo ya nje Antony Blinken na mshauri wa masuala ya usalama katika ikulu ya White House, Jake Sullivan.

Waziri wa ulinzi wa Israel Benny Gantz akihudhuria mkutano wa waandishi habari katika kambi ya kijeshi ya Kirya mjini Tel Aviv, Israel Oktoba 28, 2023
Waziri wa ulinzi wa Israel Benny GantzPicha: Abir Sultan/Pool/AP/picture alliance

Afisa mmoja mkuu kutoka chama cha Netanyahu cha mrengo wa kulia cha Likud, amesema kuwa Gantz hakupata idhini kutoka kwa Netanyahu ya mikutano yake nchini Marekani na kwamba Netanyahu alitoa onyo kwa Gantz na kusisitiza hatari ya kuongezeka kwa mpasuko katika uongozi wa ndani wa Israel wakati vita kati yake na kundi la Hamas vikiingia  mwezi wa sita.

Harris anapanga kushinikiza kuhusu kusitishwa kwa mapigano Gaza

Katika mkutano wake na Gantz, Harris anapanga kushinikiza kuweko kwa makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano ambayo yatawezesha kuachiliwa huru kwa makundi kadhaa ya mateka wanaoshikiliwa na Hamas.

Soma pia: Mashirika ya misaada yatahadharisha juu ya kuzuka baa la njaa kaskazini mwa Gaza

Siku ya Jumapili akiwa mjini Selma, Albama, nchini Marekani, Harris alisema kuwa kutokana na mateso makubwa huko Gaza, lazima kuwe na usitishaji wa mapigano mara moja kwa angalau wiki chache zijazo na kuongeza kuwa hali hii itasaidia kuachiwa huru kwa mateka na pia kufikishwa misaada kwa mamilioni ya wakaazi wa Gaza.

Watu 30,534 waripotiwa kuuawa katika vita vya ukanda wa Gaza.

Wizara ya afya huko Gaza inayodhibitiwa na Hamas, imesema leo kuwa takiban watu 30,534 wameuawa katika vita vya ukanda huo wa Gaza.

Taarifa ya wizara hiyo imesema kumekuwa na vifo 124 katika muda wa masaa 24 yaliyopita huku watu wengine 71,980 wakijeruhiwa tangu kuzuka kwa vita hivyo Oktoba 7.