1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafia katika Italy inataka kuwa na mamlaka

Othman Miraji23 Oktoba 2007

Kimsingi ilianza mwishoni mwa karne ya 19 kama nguvu dhidi ya mamlaka ya dola, lakini sasa kinachotakiwa na Mafia ni mamlaka, na hasa mamlaka ya kumiliki fedha. Italy inafahamika kama nchi mama ya mfumo wa uhalifu wa Mafia.

https://p.dw.com/p/C7rj
Wanachama wa kundi la Mafia katika Palermo, Italy, wakisindikizwa na polisi kupelekwa kizuizini
Wanachama wa kundi la Mafia katika Palermo, Italy, wakisindikizwa na polisi kupelekwa kizuiziniPicha: AP

Katika nchi hiyo yanapatikana yale majina maarufu kama Cosa Nostra au Camorra. Hivi sasa jina la DRANGEDA kutoka Calabaria ndilo linaloogopwa sana hapa Ulaya. Jörg Seisselberg ameandika juu ya kwa kiwango gani Mafia wa Italy wanavoudhibiti uchumi wa nchi hiyo.

Shirika kubwa la kibiashara la Italy, ni sio lile lenye kutengeneza magari ya Fiat, sio lile la vyombo vya habari linalomilikiwa na waziri mkuu wa zamani, Berlusconi, lakini shirika kubwa kabisa la kibiashara huko Italy ni Mafia. Shirika hilo la uhalifu linajipatia Euro bilioni 90 kwa mwaka, ni fedha nyingi sawa na mapato ya ndani ya nchi kama vile Singapore. Katika ripoti ya shirika la kupambana na Mafia la wafanya biashara wa reja reja ni kwamba Mafia inajipatia nusu ya fedha hizo kwa kuwabinya watu walipe kutokana na kulindwa ili wasidhuriwe na makundi mengine ya Mafia. Magengi ya Mafia yasingekuweko bila ya fedha yanayopata kwa kuwalazimisha watu walipe kwa kisingizio cha kuwalinda wasidhuriwe na maadui wao. Kutokana na mbinyo wa aina hiyo wa kujipatia fedha, Mafia inajinyakulia mamlaka katika maeneo Fulani.

Sio tu wenye mahoteli na mikahawa au wafanya biashara za reje reja wanaolazimishwa kutoa sehemu ya mapato yao kwa Mafia, lakini pia, na huu ni mtindo unaogopesha, hata biashara kubwa kubwa. Mafia inafanya harakati zake katika mitaa ya watu masikini huko Palermo na Neaples, na pia wahalifu wa Mafia ni wenyeji kabisa katika maofisi ya makampuni makubwa wanayofanya nayo biashara.

Rais wa heshima wa shirika la wafanya biashara za reja reja wanaopambana na Mafia, Tano Grasso: "Tusifikirie Mafia kwamba ni gengi la wahalifu wadogowadogo, lakini ni jumuiya ya kihalifu ambapo nguvu yake inatokana na kuwa na mawasiliano ya karibu sana na makampuni makubwa ya kibiashara katika maeneo yao. Na makampuni makubwa yanawalipa watu hao wenye nguvu. Baadhi ya makampuni hayo yanashirikiana na Mafia, mengine yanawastahamilia watu wa Mafia kwa kunyamaa kimya juu yale yanayotendwa. Huo, kwa bahati mbaya, ndio ukweli wa mambo na ni msingi wa sababu kwanini Mafia ina nguvu sana."

Katika ripoti ya kupambana na Mafia kumenukuliwa kisa cha kampuni ya ujenzi ya Italy, Italce-menti. Kwa mujibu wa mafaili ya uchunguzi wa polisi ni kwamba kampuni hiyo katika ujenzi wa barabara kuu baina ya Salerno na Reggio Calabria ilishirikiana na ukoo wa Mafia wa DRANGEDA. Mafia wa Calabria walikubali kwa namna hiyo kulinda visishambuliwe vifaa vya ujenzi na vitu vingine na kundi lengine la Mafia. Pia huko Calabria, na pia Sicily na katika eneo kubwa la mji wa Neaples, makamapuni mengi makubwa ya kibiashara yanaamini kwamba yataweza tu kumudu, kibiashara, ikiwa yatalipa fedha kwa Mafia au ikiwa yatashirikiana na makampuni yalioa na maingiliano na Mafia.

Tena Bwana Grasso: "Katika mikoa mingi, Mafia ndio pekee wanaodhibiti biashara, ni tuu biashara zilizo na maingiliano na Mafia, ndizo zinazoweza kutoa huduma zao. Hiyo ina maana kwamba katika mikoa hiyo ule uhuru wa kufanya biashara kwa kweli umetoweka."

Katika ripoti ya karibuni ya jumuiya wafanya biashara wa reja reja, ni kwamba huko Sicily katika kila wafanya biashara 10 basi saba wanalipa fedha ili walindwe dhidi ya mashambulio ya Mafia. Huko Calabria katika kila wafanya biashara kumi , basi watano wanafanya hivyo. Ili wajilinde na mashambulio ya makundi ya Mafia ya Cosa Nostra na yale ya DRANGEDA, inabidi maduka makubwa yalipe Euro alfu tano kila mwaka kwa wahalifu wa mpangilio, makampuni ya ujenzi yanalipa katika mahala wanapojenga Euro alfu kumi kujilinda na mashambulio ya Mafia, pia yanafanya vivyo hivyo mahoteli na vituo vinavowapokea watu watalii. Hivi sasa eneo lenye majengo ya watalii huko Sicily linamilikiwa na bosi wa Mafia. Inakisiwa kwamba uhalifu wa mpangilio unajipatia Euro bilioni saba kila mwaka kuuza bidhaa zenye nembo za uwongo ambazo zinauzwa katika maduka yanayoendeshwa kinyume na sheria na yalioko katika miji mingi ya kitalii.

Serekali ya waziri mkuu wa Italy, Romano Prodi, imetangaza kwamba katika siku chache zijazo itakuja na mkakati mpya wa usalama ambapo hatua kadhaa zitachukuliwa dhidi ya Mafia. Inapangwa kwamba serekali iweze kutwaa kwa urahisi mali za Mafia, na pia iwe vigumu zaidi kuwaacha huru kabla ya wakati wanachama wa mafia waliohukumiwa kubakia magerezani.