1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuriko Pakistan

Nina Markgraf18 Agosti 2010

Balozi wa Pakistan katika Umoja wa Mataifa aomba msaada zaidi.

https://p.dw.com/p/Oq1J
Maeneo mengi bado yako chini ya maji, Pakistan.Picha: AP

Huku hali ikizidi kuwa mbaya nchini Pakistan kufuatia mafuriko mabaya kabisa kuwahi kutokea nchini humo, jamii ya Kiislamu hapa nchini Ujerumani imeanza kuchangisha fedha kuwasaidia wahanga wa mafuriko hayo. Umoja wa Mataifa nao umesema tayari wamepata dola milioni mia mbili, nusu ya fedha zinazohitajika kwa ajili ya msaada wa kiutu kwa wahanga wa mafuriko hayo Pakistan.

Pakistan Flut Katastrophe 2010 NO FLASH
Milioni ya watu waachwa bila ya makaazi.Picha: AP

Wiki ya kwanza katika mwezi mtukufu wa Ramadhan na makundi ya kiislamu hapa nchini Ujerumani yamewatolea wito wafuasi wao, kutoa fedha kuwasadia wahanga wa mafuriko mabaya kabisa kuwahi kutokea nchini Pakistan. Inakisiwa kuwa kiasi ya watu milioni 20 wameathirika, wengi wakiachwa bila makao na mahitaji muhimu kama maji na vyakula.

Mwenyekiti wa baraza la Waislamu hapa Ujerumani Ayyub Axel Koehler amesema jamii ya waislamu hapa Ujerumani imesikitishwa mno na maafa hayo nchini Pakistan ambayo yamewaua watu kiasi ya elfu mbili. Na kama ishara kuwa wako pamoja na watu wa Pakistan, Ayub amesema kauli mbiu ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhan ni kufunga saumu, kuomba na kutoa msaada.

NO FLASH Pakistan Hochwasser Flut Hungersnot
Wanajeshi wasaidia kutoa misaada.Picha: AP

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umesema tayari umeshakusanya nusu ya fedha za msaada zinazohitajika kwa ajili ya msada wa dharura nchini Pakistan.

Kwa sasa Umoja huo umekusanya dola milioni mia mbili na nane, ambazo ni nusu ya dola milioni 460 zinazohitajika kuwasaidia wahanga wa mafuriko hayo.  Maurizio Giuliano, msemaji katika afisi inayosimamia misaada ya kiutu nchini Pakistan  amesema pia wamepokea ahadi nyingi za misaada.

Jamii ya Kimataifa imelaumiwa kwa kuzembea kutoa msaada nchini Pakistan.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki moon ambaye alizuru maeneo yaliyoathirika na mafuriko hayo nchini Pakistan, aliyataja mafuriko hayo kama janga baya kabisa kuwahi kutokea katika historia ya Pakistan.

Hadi sasa watu milioni 20 wameacha bila ya makaazi, huku maeneo mengi ya Pakistan yakiwa bado yamefunikwa na maji.

Pakistan nayo imewahakikishia wafadhili kuwa misaada hiyo ya kiutu itawafikia wahanga wa janga hilo la mafuriko, huku ikiondoa wasiwasi wa jamii ya kimataifa kuwa huenda misaada hiyo ya dharura ikaangukia mikononi mwa wanamgambao wa Taliban.

Wasiwasi wa wafadhili ni kwamba huenda misaada hiyo ya kiutu isiwafikie wanaohitaji kutokana na ufisadi serikalini pamoja na bugdha la wanamgambo wa Taliban. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi na mpango wa chakula wa Umoja huo yamesema wahanga wanakabiliwa na hali mbaya ya mateso na mahitaji makubwa, huku wataalam wa afya wakionya kuwa huenda wimbi ka pili la vifo kutokea kutokana na magonjwa ya kipindupindu na homa ya manjano.

Mwandishi: Munira Muhammad/ DPAE, DW-world

Mhariri: Mohammed AbdulRahman.