1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuriko yaendelea kutishia Pakistan.

Halima Nyanza23 Agosti 2010

Mamlaka nchini Pakistan zimekuwa zikichukua jitihada kadhaa kuweza kuuokoa maeneo yaliyoko katika jimbo la kusini mwa nchi hiyo la Sindh, baada ya wakaazi wake kuhamishwa kutokana na kitisho cha mafuriko katika eneo hilo

https://p.dw.com/p/Otwb
Mama na watoto wake wawili, wakijiokoa na mafuriko nchini Pakistan.Picha: AP

Maelfu ya watu wamehamishwa  kutoka katika maeneo yaliyo katika hatari ya kukumbwa na mafuriko kusini mwa nchi hiyo ikiwemo kutoka katika mji wa Shahdadkot, ambapo wakaazi wake wapatao 100,000 walihamishiwa katika maeneo yenye usalama.

Hata hivyo amesema bado kuna watu wamekwama katika vijiji vilivyo katika mji huo na kwamba juhudi zinafanywa kuweza kuwaokoa.

Waziri wa kilimo cha umwagiliaji katika jimbo la Sindh, Jam Saifullah Dharejo amesema kwa sasa wamekuwa wakijaribu kuulinda mji huo ambao umekumbwa na kitisho cha mafuriko.

Amesema ukuta uliojengwa  kwa ajili ya kuulinda mji huo na mafuriko uko katika hatari ya kuzolewa na maji.

Lakini amesisitiza kuwa hakuna kitisho katika mji wa Hyderabad, ambao ni wa pili kwa ukubwa katika jimbo hilo la Sindh na wa sita kwa ukubwa nchini Pakistan.

Serikali ya Pakistan imekuwa ikikabiliwa na lawama kadhaa kutokana na jinsi ilivyozubaa na jitihada za kutoa msaada, wakati maafisa nchini humo wakionya kwamba nchi hiyo inakabiliwa na hasara kubwa kiuchumi ikiwa ni hadi kiasi cha dola bilioni 42.

Mamilioni ya watu walionusurika katika janga hilo wamekuwa wakihitaji chakula, makaazi ya muda na maji safi ya kunywa na kuhitaji msaada wa kibinadamu ili kuweza kuishi, huku kukiwa na hofu ya kuongezeka kwa milipuko ya magonjwa ya maambukizo kama vile kipindupindu, ugonjwa wa matumbo na ugonjwa wa ini unaoletwa na virusi, ambao pia unaambukiza.

Msemaji wa kitengo kinachoratibu masuala ya kiutu katika ofisi za Umoja wa mataifa mjini Islamabad Maurizio Giuliano amesema leo kwamba  watu milioni moja na nusu wamebata matibabu kutokana na magonjwa ya kuambukiza ya ngozi.

Nalo shirika la fedha la Umoja wa Mataifa -IMF- leo linatarajia kuanza mazungumzo na maafisa wa Pakistan kurekebisha tena mkopo wa dola bilioni 10.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon ameitaka jumuia ya kimataifa kutoa msaada wa haraka wa karibu dola milioni 500 kwa Pakistan na kuonya kwamba nchi hiyo inahitaji pia msaada wa muda mrefu.

Takriban wat 1,500 wamekufa na wengine milioni 20 wameathiriwa na janga hilo baya la mafuriko kuwahi kuikumba nchi hiyo, huku kitisho cha magonjwa ya kuambukiza kikizidi kuongezeka katika kambi wanazoishi watu walionusurika na janga hilo.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed