1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuriko yaikumba Pakistan.

Halima Nyanza2 Agosti 2010

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesikitishwa mno na kuongezeka idadi ya watu waliokufa kutokana na mafuriko yaliyoikumba Pakistan na kuahidi msaada zaidi kutoka Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/OZpY
Wanavijiji wa Pakistan wakihangaika kujiokoa na mafuriko.Picha: ap

Serikali ya Pakistan inaendelea na juhudi za kuwahudia wahanga huku nchi za kigeni zikiahidi kuwapeleka misaada ya kibinadamu.

Katika taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa, msemaji wa Katibu Mkuu amesema kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amehuzunishwa na vifo vya watu kutokana na mafuriko hayo pamoja na wengine kupoteza kazi zao pamoja na miundo mbinu kutokana na mvua zilizonyesha hivi karibuni nchini Pakistan ambazo zimesababisha mafuriko mabaya kabisa kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 80 iliyopita na kuathiri zaidi ya watu milioni moja.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameidhinisha tayari kiasi cha hadi dola milioni 10 kutoka katika mfuko wa dharura kwa ajili ya kusaidia mahitaji mbalimbali kwa watu walioathiriwa na mafuriko.

Hata hivyo Manuel Bessler kutoka katika ofisi za Umoja wa Mataifa nchini Pakistan zinazoshughulikia masuala ya kibinadamu, anasema huduma za usambazaji misaada zimekuwa zikikwamishwa na miundo mbinu iliyoharibiwa na mafuriko hayo.

Nalo jeshi la anga la Pakistan limesema kuwa limewachukua zaidi ya watu 500 waliokuwa wamekwama, wakiwemo raia wa kigeni sita, ikiwa kama sehemu ya uokoaji.

Idadi ya waliokufa mpaka sasa katika mafuriko hayo mabaya kuwahi kuikumba Pakistan imefikia 1,100, huku magonjwa yanayoenezwa kupitia maji machafu yakilipuka na kuwa tishio kubwa kwa waathirika.

Nchi na jumuiya mbalimbali tayari zimetangaza kutoa msaada wa fedha kuisaidia nchi hiyo.

Serikali ya Marekani, mshirika mkubwa wa Pakistan katika vita dhidi ya Ugaidi imetangaza kutoa kiasi cha dola milioni 10 huku ikiwa imetuma helikopta na boti nchini Pakistan.

China, nchi ambayo mara kadhaa imekumbwa na mafuriko imetangaza mchango wa kiasi cha milioni moja na nusu.

Kwa upande wake, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Bernard Kouchner ameelezea mshikamano ilioweka Ufaransa katika kukabiliana na mafuriko hayo.

Akielezea athari za mafuriko hayo, Waziri wa Habari katika  jimbo la kaskazini magharibi la Khyber Pakhtunkhwa, nchini Pakistan, Iftkhar Hussain amesema bado wamekuwa wakipokea taarifa juu ya watu waliopoteza maisha na mali zao kutokana na mafuriko hayo katika sehemu mbalimbali za jimbo hilo na kwamba anahofia kuwa idadi ya watu waliokufa inaweza kuongezeka.

Amesema zaidi ya nyumba 3,700 zimesombwa na maji na idadi ya watu walioachwa bila ya makaazi ikizidi kuongezeka.

Zaidi ya watu milioni moja na nusu wameathiriwa na mafuriko pamoja na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua za msimu katika jimbo la kaskazini magharibi mwa Pakistan.

Mafuriko hayo pia yamezikumba sehemu za Afghanistan na kusababisha vifo vya watu 65 huku familia zaidi ya 1,000 zikiathiriwa.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri:Josephat Charo