1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazeti ya Ujerumani yazungumzia madhila ya Waafrika walioko Israel

Abdu Said Mtullya11 Juni 2012

Magazeti ya Ujerumani yamezungumzia matatizo yanayowakabili wakimbizi 60,000 kutoka Afrika nchini Israel, wizi wa fedha Sudan ya Kusini na mgawanyiko miongoni mwa Wamisri kabla ya duru ya pili ya uchaguzi wa urais.

https://p.dw.com/p/15C4c
Wakimbizi wa Kiafrika nchini Israel.
Wakimbizi wa Kiafrika nchini Israel.Picha: picture-alliance/dpa

Gazeti la "Berliner Zeitung" limechapisha makala juu ya wakimbizi wa Kiafrika waliopo nchini Israel. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba wakimbizi alfu 60 kutoka Sudan na Eritrea wamengia Israel, lakini hakuna anaewakaribisha. Gazeti hilo linaeleza katika makala yake kuwa wakimbizi zaidi ya 60,000, wengi wao kutoka Sudan na Eritrea, wamekwama nchini Israel. Wengi wao wamepitia mitihani mikubwa.

Lakini hakuna hata mmoja anaetambuliwa kuwa mkimbizi na Israel. Sera ya Israel kuhusu wakimbizi hao ni kuonyesha kwamba watu hao hawakaribishwi nchini. Wakimbizi hao kutoka Afrika wanaitwa "Mistaninim" yaani watu waliojipenyeza. Gazeti la "Berliner Zeitung" limearifu katika makala yake kwamba idadi ya wakimbizi wa Kiafrika wanaoingia Israel kwa kupitia Sinai imeongezeka kwa kiwango kikubwa hivi karibuni.

Gazeti la "Süddeutsche Zeitung" limechapisha makala juu ya wizi wa fedha katika Sudan ya Kusini. Gazeti hilo limearifu katika makala yake kwamba kiasi cha dola Bilioni nne kimeibiwa na sasa Rais wa nchi hiyo Salva Kiir amewaandikia barua mawaziri wake na watumishi wengine wa serikali walioziiba fedha hizo wazirudishe.

"Süddeutsche Zeitung" limeandika kuwa Rais Salva Kiir amechukua hatua kufuatia shinikizo la Marekani mfadhili mkuu wa Sudan ya Kusini. Marekani imempa Rais huyo nyaraka zenye majina ya watu waliohusika na wizi wa hizo dola bilioni nne. Kutokana na shinikizo hilo Rais Kiir amewaandikia barua mawaziri wake na watumishi wengine wa serikali kuwakumbusha kwamba watu wa Sudan ya Kusini wanakabiliwa na dhiki kubwa lakini baadhi ya viongozi wanajitajirisha.

Gazeti la "Suddeutsche Zeitung" limeipata nakala ya barua ya Rais Salva Kiir. Katika barua hiyo anasema kuwa watu wa Sudan ya Kusini walipigana ili kujikomboa na kuwa huru na kuleta haki. Lakini sasa baada ya kuingia katika madaraka viongozi wameyasahau malengo hayo, na badala yake wanajitajirisha. Gazeti hilo limemnukuu waziri wa mambo ya ndani Barnaba Marial Benjamin akisema kuwa nusu ya fedha hizo zilipotokea kuhusiana na nafaka hewa.

Rais Salva Kiir Mayardit wa Sudan ya Kusini.
Rais Salva Kiir Mayardit wa Sudan ya Kusini.Picha: picture alliance / ZUMA Press

Mkuu wa Kanisa Katoliki katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kadinali Laurent Monsengwo, amezikosoa taratibu zilizotumiwa na tume huru ya uchaguzi wakati wa uchaguzi mkuu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Gazeti la "Die Tageszeitung" limemnukuu Kadinali huyo alipotoa hotuba mjini Berlin.

Kadinali Monsengwo amesema katika hotuba ya kupokea tuzo ya kanisa na amani mjini Berlin kwamba uamuzi wa wapiga kura unapaswa kuheshimiwa la siyvo itakuwa vigumu kuleta maridhiano katika nchi. Gazeti la "die tageszeitung" limeeleza kuwa kauli ya kadinali Monsengwo inatokana na hatua iliyochukuliwa katika Jamhuri ya Kisdemokrasi ya Kongo yenye lengo la kuleta mageuzi katika tume ya uchaguzi ili kuzuia udanganyifu wakati wa kuhesabu kura.

Mbunge wa upinzani Emery Okunji amewasilisha mswada wa mageuzi ya tume hiyo - CENI ili kuzuia udanganyifu. Pamoja na mageuzi hayo ni kuzijumuisha pia asasi za kiraia katika tume hiyo, na ikiwezekana kundi lao litapaswa liwe kubwa kuliko jumuiya nyingine katika tume. Mpaka sasa waliomo katika tume huru ya uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ni wawakilishi wa serikali na wa vyama vya upinzani.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine"linazungumzia juu ya matukio ya nchi Misri baada ya kufanyika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais na baada ya Mahakama kumhukumu Rais wa hapo awali Hosni Mubarak kifungo cha maisha jela. Mwandishi wa makala ya "Frankfurter Allgemeine" anaeleza kuwa Wamisri wanaendelea na maandamano ya kupinga hukumu zilizotolewa dhidi ya Mubarak na watoto wake. Wengine wanapinga kushiriki kwa Shafiq katika kugombea urais kwani alikuwa waziri Mkuu wakati wa Mubarak.

Waandamanaji nchini Misri wakipinga adhabu "ndogo" ya kifungo cha maisha aliyopewa Hosni Mubarak.
Waandamanaji nchini Misri wakipinga adhabu "ndogo" ya kifungo cha maisha aliyopewa Hosni Mubarak.Picha: Reuters

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasena walioshindwa katika duru ya kwanza ya uchaguzi ni wamisri wote waliotaka mabadiliko ya haraka baada ya Mubarak kutimuliwa.

Mwandishi: Abdu Mtullya/Deutsche Zeitungen
Mhariri: Josephat Charo