1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

P.Martin16 Juni 2008

Pendekezo la chama cha SPD kurefusha mpango wa kuwabakisha kazini kwa nusu mkataba waajiriwa wanaokaribia kustaafu ni miongoni mwa habari zilizogonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/EKTX

Lakini hebu tuanze na matokeo ya kura ya maoni iliyopigwa nchini Ireland kuhusu mkataba mpya wa Ulaya.Gazeti la OSNABRÜCKER ZEITUNG kutoka Mainz linasema:

Kilichotokea wala hakishangazi,kwani Umoja wa Ulaya umepanuka kwa haraka bila ya hata kuhakikisha hapo kabla kuwa wanachama wote 27 watakuwa na uwezo wa kuafikiana.Sasa ni vigumu zaidi kwa umma kuamini kuwa mkataba huo mpya wa Umoja wa Ulaya wenye azma ya kuleta mfungamano zaidi kati ya wanachama wake, utawanufaisha raia.

MOD: ALLGEMEINE ZEITUNG likiendelea na mada hiyo hiyo linasema:

Kwa wengi Brussels,makao makuu ya Umoja wa Ulaya ni adui mkubwa anaeogopwa.Sababu mojawapo ni jinsi umoja huo ulivyokuwa kwa haraka na ukweli kwamba hivi karibuni Bulgaria na Rumania zilikaribishwa katika Umoja wa Ulaya bila ya nchi hizo hata kutimiza masharti ya uanachama.

Je,mkasa uliotokea Ireland humaanisha mwanzo wa kusambaratika kwa muundo wa Umoja wa Ulaya uliokuwepo hadi hivi sasa?Hilo ni suala linaloulizwa na LANDESZEITUNG LÜNEBURG.

likiiendelea linasema,ikiwa Umoja wa Ulaya katika siku zijazo unataka kuwa na umoja halisi wa mataifa mbali mbali na sio tu soko la pamoja la kiuchumi,basi umoja huo unapaswa kueleza wazi wazi wajibu wake na sio malengo yake tu.

Sasa hebu tutupie jicho mada iliyosababisha midahalo mikali huku Ujerumani ambako idadi ya wastaafu inaongezeka wakati ya wenye ajira na kulipa kodi inapunguka.Gazeti la KIELER NACHRICHTEN linasema:

Kimsingi ni barabara kuwaastaafisha waajiriwa hatua kwa hatua.Ni wajibu wa serikali kuzalisha nafasi mpya za ajira kwa njia hiyo badala ya kuwashinikiza kustaafu na hatimae serikali kuishia kubeba mziigo wa kulipa pesa nyingi.

Lakini gazeti la KÖLNISCHE RUNDSCAHU lina maoni tofauti,kwani linasema hivi:

Ni kosa kubwa kuamini kuwa kwa kuwapunguzia kazi waajiriwa wanaokaribia kustaafu,kutazalisha nafasi mpya za ajira kwa vijana.Kwa maoni ya KÖLNISCHE RUNDSCHAU,kuzingatia kuutekeleza utaratibu huo kwa wafanyakazi kuanzia umri wa miaka 60,ni kushambulia mpango mpya wa kustaafu kwa umri wa miaka 67.

Mada nyingine inayogonga vichwa vya habari tangu muda mrefu ni vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran kuhusika na mradi wake wa nyuklia.Gazeti la HAMBURGER ABENDBLATT linasema:

Hakuna anaeamini kuwa mripuko wa bei ya mafuta unailazimisha Iran kugeukia nishati ya nyuklia.Ni dhahiri kuwa China sasa itaupiku Umoja wa Ulaya kama mshirika mkuu wa Iran katika sekta ya biashara.Hadi hivi sasa China ilisita kuunga mkono vikwazo dhidi ya Iran.Lakini michezo ya Olimpiki ikikaribia,ni dhahiri kuwa China haitaki kuzihamakisha nchi za Umoja wa Ulaya.Kwa hivyo kuna uwezekano mzuri wa kupatikana msimamo mmoja katika suala la kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi,lamalizia HAMBURGER ABENDBLATT.