1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

Prema Martin24 Februari 2010

<p>Kisa cha Askofu aliekutikana akiendesha gari huku kalewa na mkasa wa kutoa fedha ili kuweza kuonana na waziri mkuu wa mkoa wa North Rhein Westphalia ni mada zilizogonga vichwa vya habari magazetini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/M9rp
Basi tutaanza na kisa cha Askofu Margot Käßmann. Gazeti la NORDWEST-ZEITUNG linasema:

"Katika maisha yake, Askofu Margot Käßmann wa Kanisa la Kilutheri la mji wa Hannover, amekumbana na misukosuko ya kuugua saratani na ndoa yake kuvunjika. Je, safari hii kiongozi huyo wa Makanisa ya Kiinjili nchini Ujerumani atanusurika na kisa hiki cha kuendesha gari akiwa ameelewa? Bila shaka wapinzani wake wanachekelea kwani kisa hicho kimewapa nguvu kutoa madai ya kumtaka ajiuzulu."

Likiendelea linasema:

"Hata kiongozi wa kanisa ni binadamu anaeweza kufanya kosa, lakini maadili yake ni ya juu zaidi kulinganishwa na viongozi wengine katika jamii. Isitoshe, Askofu huyo ni maarufu na anaogopwa kwani yeye hachelei kusema ukweli kama ulivyo.Sasa ndio inambidi mwenyewe atafakari."

REUTLINGER GENERAL-ANZEIGER likiandika juu ya mada hiyo hiyo linasema:

"Hasa yule anaemlinganisha Askofu Käßmann na maadili ya Kikristo anaweza kufanya hivyo kwa faraja. Kwani la muhimu zaidi ni huruma,usuluhifu na kukiri kuwa kufanya makosa ni ubinadamu. Ikiwa,mara kwa mara  Askofu Käßmann atakumbushwa makosa aliyofanya, basi mtaalamu huyo wa dini mwenye sifa, huenda akaamua mwenyewe kujiuzulu. Na hali hiyo itasababisha hasara sio tu kwa kanisa lake bali kwa jamii nzima." 

Tukipindukia mada inayohusika na kisa cha kutoa fedha ili kupata fursa ya kuonana na waziri mkuu wa mkoa wa North Rhine Westphalia, gazeti la MANNHEIMER MORGEN linaandika:

" Kwa mujibu wa Katiba, wabunge hawalazimiki kufuata mwongozo. Wanaokejeli wanaongezea: isipokuwa malipo yanapohusika.Je, huo ni mzaha mbaya? Peke yake dalili ya kuwepo mtindo wa nipe nikupe inastahiki kuchukuliwa hatua, kwa sababu anaeshawishi maamuzi ya serikali kwa kutoa pesa anakiuka Katiba. Kwa hivyo sasa makampuni na mashirika yapigwe marufuku kutoa michango ya pesa kwa vyama vya kisiasa."

Mwandishi: Martin,Prema/DPA

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed