1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

10 Machi 2010

Mivutano ya serikali ya muungano na uamuzi wa Mahakama Kuu kuendelea kuwafunga wahalifu kwa sababu za usalama, hata baada ya kukamilisha adhabu ya kifungo ni mada zilizochomoza katika magazeti ya Ujerumani leo hii.

https://p.dw.com/p/MOk7

Tukianza na uamuzi wa Mahakama Kuu uliozusha mabishano mapya, gazeti la STUTTGARTER NACHRICHTEN linaandika:

"Kimsingi wale wasiohusika, ndio wanaokosoa na kusema kuwa hakuna binaadamu anaestahiki kuadhibiwa mara mbili na kuendelea kuwekwa kizuizini. Huo ni ukatili. Lakini gazeti hilo linasema, ukweli ni kuwa wakosoaji hao ndio wanaoonyesha ukatili. Kwani, kila miaka miwili huchungzwa ikiwa wahalifu hao waendelee kuzuiliwa kwa usalama wa jamii. Na wahalifu vijana wanapohusika, basi uchunguzi huo hufanywa kila mwaka. Kwa hivyo, hakuna adhabu ya mara mbili, bali umma unalindwa dhidi ya wahalifu hao ikiwa wao bado ni hatari  kwa jamii."

Kwa upande mwingine,gazeti la SAARBRÜCKER ZEITUNG likiunga mkono uamuzi wa Mahakama Kuu linasema:

"Uhalifu unapopindukia, basi mahakama haina budi kuchukua hatua kali. Na wakati mwingine, njia pekee ya kuilinda jamii, hasa dhidi ya wahalifu hatari, ni kuwafunga wahalifu hao kwa daima. Na hiyo iweze kufanywa bila ya kuzingatia umri wa mhalifu, kama ilivyothibitishwa na Mahakama Kuu. Kwani hatari haihusiki na umri wa mtu."

Tukigeukia mada nyingine, gazeti la HANNOVERSCHE ALLGEMEINE ZEITUNG limeandika:

"Kwa majuma kadhaa ilionekana kana kwamba serikali mpya ya muungano wa nyeusi na manjano yaani vyama vya kihafidhina CDU/CSU na kiliberal FDP, haikutaka na haikuweza kuongoza, badala yake ilikuwa ikizozana tu. Sasa yaonekana kuwa matamshi yamepungua makali na njia ipo wazi kushughulikia masuala magumu serikalini."

"Je, hiyo ni kwa sababu Guido Westerwelle hayupo nchini kwa sababu ya ziara yake ndefu katika Amerika ya Kusini kama wengine wanavyotania?"

Angalao moja limedhihirika: serikali ya muungano wa nyeusi na manjano, hivi sasa haishughulikii tu mivutano ya ndani ya kuania madaraka. Washirika hao wepya wameanza kutawala."

Tunamalizia kwa mada inayoendelea kugonga vichwa vya habari magazetini: mzozo wa fedha wa Ugiriki ulioathiri pia thamani ya sarafu ya Euro. Gazeti la  COBURGER TAGEBLATT likieleza maoni yake kuhusu pendekezo la Umoja wa Ulaya la kutaka kuunda Shirika  la Fedha la Ulaya linaandika:

"Kuunda taasisi maalum kwa sababu ya vitendo vya kutowajibika na kuvumilia vitendo hivyo ,ni jambo lisiloweza kukubaliwa hata kidogo. Kwani serikali zilizoangusha uchumi wa nchi kwa sababu ya kuwa na uongozi mbaya, hazipaswi kutunzwa kwa mikopo."

Mwandishi:Martin,Prema/DPA

Mhariri: Charo,Josephat