1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

9 Septemba 2010

Na sasa ni wakati wa kuchambua habari zilizogonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/P7g2

Wito wa kuchoma Quran ulitolewa na padri wa Kimarekani na tuzo ya vyombo vya habari aliopewa mchoraji wa katuni zilizomkashifu Mtume Mohamed ni mada kuu zilizoshughulikiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani Alkhamisi ya leo. Magazeti mengine yakiunga mkono kumpa mchoraji Kurt Westergaard kutoka Denmark tuzo hiyo mengine yanapinga uamuzi wa kumpa tuzo hiyo.

Basi tutaanza na gazeti la HESSISCHE-NIEDERSÄCHSISCHE ALLGEMEINE linalosema:

"Kisiasa, si busara kumtukuza kama kitambulisho cha uhuru wa kutoa maoni, mchoraji aliemkashifu Mtume Mohamed. Mtu apaswa kuzingatia hisia za wengine.Pindi Kurt Westergaard angemchora Yesu Kristo kama gaidi wa kimamboleo, basi yeye asingeangaliwa kama ni mwenye kustahiki kupewa zawadi hiyo."

Kwa upande mwingine gazeti la WESER KURIER linaandika:

"Westergaard hakumtusi mtu ye yote kwa sababu ya asili yake au dini, seuze kumtisha. Hajavunja sheria isipokuwa ameitumia ipasavyo. Pekee ukweli kuwa tangu wakati huo amekuwa akitishiwa kuuliwa na wafuasi wa itikadi kali, inatosha kuhalalisha kumuunga mkono. Ikiwa Kansela anashiriki katika hafla ya kumtukuza na mgombea wa zamani wa urais Joachim Gauck, akihotubia sherehe hiyo, basi hiyo ni ishara bayana na inayofaa. Uhuru wa mtu kutoa maoni yake ni haki ya binadamu kote ulimwenguni na ni suala lisilojadilika kwa vyo vyote vile."

Sasa tunapindukia mada nyingine inayoendelea kugonga vichwa vya habari. Kwa maoni ya gazeti la REUTLINGER GENERAL ANZEIGER, wito wa padri wa Marekani kuchoma moto kitabu kitukufu cha Waislamu - Quran ni tusi kwa Waislamu wote. Likiendelea linauliza:

"Je,Wakristo wangesemaje kama Biblia ndio ingelipigiwa upatu kutiwa moto kwa mito kama hiyo ya kijinga na karaha?"

Na gazeti la RECKLINGHÄUSER ZEITUNG linasema:

"Padri Terry Jones ni mfuasi wa itikadi kali sana. Ni vyema kuwa viongozi wa kidini wa Wayahudi, Wakristo na Waislamu kwa kauli moja, wamelaani mpango huo wa aibu. Hapo, watu wanabidi kukumbuka yaliyosemwa na Heinrich Heine mnamo mwaka 1820: kwamba mtu akitia moto vitabu anawatia moto binadamu - matamshi ambayo pia yanahusiana na kutiwa moto Quran eneo la Granada nchini Uhispania ilipotekwa na Wakristo."

Mwandishi:P.Martin/DPA

Mhariri: M.Abdul-Rahman