1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

7 Oktoba 2010

Mradi wa ujenzi wa reli na kituo kipya cha treni katika mji wa Stuttgart kusini mwa Ujerumani na wasiwasi kuhusu afya ya Waziri wa Fedha wa Ujerumani ni baadhi ya mada zilizochambuliwa katika magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/PY0Z

Basi tutaanza na mada iliyo maarufu kama "Stuttgart 21" yaani ujenzi wa reli ya Stuttgart katika jimbo la kusini la Baden Württemberg. Gazeti la RHEIN-NECKAR ZEITUNG linasema:

"Kumteua mwanasiasa mkongwe Heiner Geißler wa chama cha kihafidhina cha CDU, kama mpatanishi katika mvutano wa Stuttgart 21, ni uamuzi ulio bora kuliko maamuzi mengine yaliyopitishwa na Waziri Mkuu Stefan Mappus wa jimbo la Baden Württemberg katika miezi ya hivi karibuni. Kwani Geißler mwenye msimamo wa wastani wa kihafidhina ni mwanasiasa aneheshimiwa katika kila kambi."

Lakini gazeti la STUTTGARTER NACHRICHTEN linaamini vingine:

"Hata kwa Geißler, uwezo wa kupata maafikiano ni mdogo. Wapinzani wa mradi wa Stuttgart 21 hawataki tu kushirikishwa katika maamuzi ya ujenzi wa reli hiyo kama mwanasiasa wa chama cha Kijani alivyoeleza hiyo jana. Wao wanataka kuufutilia mbali mradi huo wakati serikali ya jimbo ikisema kuwa imedhamiria kusonga mbele na ujenzi wa reli hiyo. Kwa hivyo licha ya Geißler, mvutano huo utabakia pale pale. Kila upande unanyosha mkono,lakini hakuna aliebadili msimamo wake. Ionekanavyo, hatima ya mradi huo huenda ikaamuliwa katika uchaguzi wa jimbo hilo utakaofanywa mwezi Machi mwakani."

Lakini gazeti la SCHWÄBISCHE ZEITUNG linasema:

"Uchaguzi wa jimbo kufanywa kuwa kura ya maoni kuhusu ujenzi wa reli hiyo ya Stuttgart ni jambo la hatari. Kwani uchaguzi huo upo mbali na hali inazidi kutokota katika mji mkuu wa jimbo la Baden-Württemberg. Hata hivyo ,mvutano huo usigubike masuala mengine muhimu katika uchaguzi huo wa Machi 27. Moja ni dhahiri, ujenzi wa reli hiyo ya Stuttgart utazidi kuchelewa na hiyo itasababisha gharama zaidi. Lakini hasara watakayopata wanasiasa haiwezi kukadiriwa kwa hivi sasa."

Tukigeukia mada nyingine, gazeti la NÜRNBERGER NACHRICHTEN linaandika:

"Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble ni mtu mwenye hadhi na sifa za kipekee – ambazo siku hizi ni nadra sana kukutikana katika ngazi za juu. Lakini afya ya waziri huyo imezusha wasiwasi na wananchi wake wanataka kujua ukweli. Je, afya yake inamruhusu kubakia kazini au la? Hakuna mwengine isipokuwa Schäuble mwenyewe anaeweza kujibu suala hilo. Ikiwa atajiuzulu, basi hilo litawasikitisha wengi, lakini kila mmoja ataheshimu uamuzi wake" lamalizia NURNBERGER ZEITUNG.

Mwandishi.P.Martin

Mpitiaji:Charo,Josephat