1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

14 Oktoba 2010

Wachimba migodi waliookolewa nchini Chile baada ya kunasa katika mgodi kwa siku 69 ndio mada iliyoshughulikiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii.

https://p.dw.com/p/Pe52

Mada nyingine inayoendelea kushughulikiwa na wahariri hao inahusika na mradi wa utata wa ujenzi wa kituo cha treni na reli maarufu kama "Stuttgart 21". Basi tukianza na muujiza uliotokea Chile gazeti la BILD linaandika:

"Kote duniani watu walifurahia kuona wachimba migodi walionasa kiasi ya mita 700 chini ya ardhi kwa siku 69 wakitolewa nje mmoja baada ya mwingine. Muujiza huo wa Chile uliwasisimua walimwengu. Kuanzia sasa, sote tunapaswa kuheshimu zaidi kazi ya wachimba migodi na tuwatakie kila la kheri."

Gazeti la SÜDKURIER likiendelea na mada hiyo hiyo linasema:

"Picha zilizoonyesha sura za wachimba migodi zenye furaha na machozi zitabakia vichwani mwetu kwa muda mrefu. Kilichotokea katika mgodi wa Chile kimeonyesha uwezo wa binadamu panapokuwepo mshikamano. Familia za wachimba migodi ziliungwa mkono na kila mmoja bila ya kubaguana- kuanzia majirani,marafiki hadi wanasiasa. Na hiyo katika nchi inayoendelea kuathirika na enzi ya utawala wa kidikteta wa Pinochet iliyotenganisha jamii. Kwa mara ya kwanza, Wachile wameona jinsi nchi yao inavyoweza kukabiliana na hali ya hatari, wananchi wanaposhikamana."

Gazeti la SAARBRÜCKER ZEITUNG linasema: Vile wataalamu wa kimataifa walivyoshiriki katika jitahada za kuwaokoa wachimba migodi wa Chile ni mfano mzuri wa utandawazi. Je,hiyo ni ajabu?

"Jawabu ni la. Ingekuwa ajabu kwa mfano kama mamilioni ya watu walioufuatiliza mkasa huo katika televisheni, wangetaka kujua kile kilichosababisha ajali ya mgodi huo. Kkwa mfano kujiarifu juu ya mazingira magumu ya kazi ya wachimba migodi na sio ya Wachile hao tu bali hata maelfu ya wachimba migodi katika nchi zinazoendelea na zinazoinukia kiuchumi. Wangejiarifu kuhusu uzembe unaofanywa na makampuni ya madini kuanzia Amerika ya Kusini hadi barani Afrika,nchini Urusi na China kwa azma ya kuongeza faida wanayopata. Au wanageuliza nani atakaelipa gharama za mamilioni za kuwaokoa wachimba migodi hao. Italipa kampuni ya madini San Esteban au mara nyingine tena walipa kodi ndio watakaotwikwa mzigo huo."

Sasa tukitupia jicho mada nyingine gazeti la BERLINER ZEITUNG linaandika:

"Walionufaika kutokana na mzozo wa "Stuttgart 21" ni walinzi wa mazingira yaani chama cha Kijani. Kwani kwa mara ya kwanza katika historia yake kuna uwezekano wa kushinda katika jimbo la Baden-Württemberg na hata huenda kikakipiku chama cha SPD. Yafurahisha kuona chama cha SPD kikitamka wazi wazi kwamba ni bora kuwa mshirika mdogo wa chama cha Kijani kuliko kushiriki katika serikali ya muungano wa vyama vikubwa chini ya uongozi wa Stefan Mappus wa kihafidhina. Kwa matamshi hayo,chama cha Kijani kimepachikwa jukumu la kuwavutia wapiga kura wa kutosha ili serikali ya kwanza ya vyama vya Kijani na SPD iweze kuundwa katika jimbo hilo kufuatia uchaguzi wa Machi 27."

Mwandishi:P.Martin/DPA

Mpitiaji:M.Abdul-Rahman