Maoni ya wahariri.
10 Aprili 2008
Wajerumani bado wanajadili mkasa unaohusu mafunzo yaliyotolewa na maafisa Ujerumani kwa polisi wa Libya. Serikali ya Ujerumani imejitetea kwa kusema kuwa mafunzo hayo yalitolewa na kampuni ya watu binafsi. Lakini juu ya hayo mhariri wa gazeti la RHEIN-NECKER anauliza kwa nini hapakutolewa taarifa yoyote.?
Masuala mengine yanayozungumziwa na wahariri leo ni juu ya Irak ,na wasiwasi uliopo nchini Ujerumani juu ya kiwango cha elimu miongoni mwa baadhi ya vijana.
Na gazeti la BERLINER ZEITUNG linazungumzia juu ya mwenge wa olimpiki. Gazeti hilo linasema maandamano yanayofanyika kupinga mwenge wa olimpiki, hayaelekezwi tu dhidi ya kukiukwa haki za binadamu nchini China. Mhariri anaeleza kuwa maandamano hayo yanaonesha taharuki iliyopo juu ya sera ya dunia utandawazi ambayo ,kwa mtazamo wa nchi za magharibi inawakilishwa kwa uthabiti na China.
Aghalabu China inaonekana kuwa tishio na mshindani mkali katika kuwania raslimali kama ,vile mafuta na madini.
Mhariri wa gazeti la BERLINER ZEITUNG anaeleza katika maoni yake kuwa nchi za magharibi zina wasiwasi juu ya China.
Gazeti hilo linamaliza maoni yake kwa kusema kwamba mayowe yanayopigwa juu ya kukiukwa haki za binadamu nchini China,ni usafidi-ni kisingizio cha kusema kuwa China imo njiani kuzipita nchi za magharibi katika kuidhibiti dunia mnamo karne hii.
Magazeti ya Ujerumani leo pia yanazungumzia juu ya Irak.
Gazeti la Swäbische Zeitung linasema katika maoni yake, Marekani lazima ifafanue vizuri malengo yake nchini Irak ,la sivyo kinachotokea sasa kitageuka kuwa zoezi la kudumu.
Gazeti linasema ukweli, ni kwamba Irak haitakuwa kigezo cha demokrasia.
Kinachotakiwa,gazeti linasema, ni kuhakikisha kuwa nchi hiyo haigeuki kuwa tishio kwa jirani zake.
Lakini hayo yanaweza kufikiwa kwa mapatano baina ya Irak na jirani zake.
Gazeti linasema mtu yeyote kutoka nje, hatasaidia.
Gazeti la CELLESCHE ZEITUNG
linasisitiza yaliyosemwa na shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo OECD , kuwa Ujerumani inapaswa kufanya mageuzi katika sekta ya elimu. Gazzeti hilo linatilia maanani kwamba Ujerumani inapuuza mustakabal wake kutokana na sera hafifu ya elimu.
Gazeti linasema viwanda na mashirika yanalalamika kuwa vijana wengi hawawezi kusoma na kandika vizuri.
Kutokana na hali hiyo gazeti la CELLESCHE ZEITUNG linaitaka serikali iekeze fedha zaidi katika sekta ya elimu-
kwani huo ndiyo msingi wa maendeleo ya siku za usoni.