1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri.

Mtullya, Abdu Said3 Juni 2008

Magazeti ya Ujerumani leo pamoja na masuala mengine yanazungumzia juu ya shambulio la bomu kwenye ubalozi wa Denmark mjini Islamabad.

https://p.dw.com/p/EBtu
Shambulio la bomu kwenye ubalozi wa Denmark mjini IslamabadPicha: AP


Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya shambulio la bomu kwenye ubalozi wa Denmark mjini Islamabad na juu ya sheria ya uhamiaji nchini Uswis.

Wahariri hao pia wanatoa maoni yao juu ya masuala ya ndani ya Ujerumani ikiwa pamoja na mgomo wa wazalishaji maziwa na kashfa ya ujasusi iliyotokea kwenye shirika la simu, Telekom.

Juu ya shambulio la bomu kwenye ubalozi wa Denmark mjini Islamabad mhariri wa gazeti la Kieler Nachrichten anasema shambulio hilo linathibitisha mambo mawili -kwanza chuki ya wanaitikadi kali wa kiislamu dhidi ya kitu chochote cha magharibi, na pili linathibitisha kushindwa kwa serikali ya Pakistan kuwadhibiti magaidi.Na mhariri wa gazeti la Westfälische Nachrichten anaongeza kwa kusema:Kwamba tukio hilo siyo la mwisho.Sababu ni kuwa wanaitikadi kali wa kiislamu wanataka watu wakati wote wakumbuke juu ya vibonzo vilivyochapishwa katika magazeti ya nchini Denmark ,kumdhihaki mtume wa dini ya kiislamu.

Gazeti la Main Echo linazungumzia juu ya sheria ya uhamiaji nchini Uswis.Gazeti hilo linasema Uswis itapaswa kuamua mwaka ujao iwapo itaacha mipaka yake wazi kwa wanachama wapya wa Umoja wa Ulaya yaani Bulgaria na Rumania. Ikiwa itafanya hivyo, mipaka baina yake na Umoja wa Ulaya itaendelea kuwa wazi kama ilivyo hadi hivi sasa.

Magazeti ya Münchner Merkur na Hannoversche yanazungumzia masuala ya ndani ya Ujerumani- juu ya mgomo katika sekta ya maziwa na kashfa ya ujasusi iliyotokea katika kampuni ya simu -Telekom ya Ujerumani.Kashfa hiyo inahusu mameneja,wafanyakazi wengine wa kampuni na waandishi habari waliopelelezwa.

Mhariri wa gazeti la Münchner Merkur anasema licha ya kashfa hiyo kuwa kubwa,serikali ya Ujerumani inarudi nyuma katika kuchukua hatua; gazeti linaeleza,sababu ni kwamba serikali hiyo ndiyo yenye hisa kubwa zaidi katika kampuni. Kuhusu mgomo wa wazalishaji maziwa gazeti la Hannoversche linasema haitakuwa sawa kwa wazalishaji maziwa hao kuendelea kupata hasara wakati wenye maduka ya kati wanaendelea kujinufaisha kwa kupandisha bei ya maziwa.Lazima suluhisho lipatikane ili kumaliza mgomo.