1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magipsi wafukuzwa Ufaransa

Miraji Othman13 Agosti 2010

Magipsi wa Rumania na Bulgaria wafukuzwa Ufaransa

https://p.dw.com/p/OnEZ
Familia ya Magipsy katika kambi yao huko Saint Denis, kaskazini ya mji wa ParisPicha: AP

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa July, serekali ya Ufaransa ilitangaza itakabiliana barabara na makaazi yasiokuwa halali ya Magipsi. Mnamo wiki mbili makambi 40 ya watu hao yametoweka. Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa, Brice Hortefeux, alitangaza kwamba magipsi 700 waliotokea Bulgaria na Rumania watarejeshwa makwao mwezi huu. Vitu vyao wamevitia katika mifuko na vijigari vya kubebea bidhaa masokoni. Hivi sasa wakaazi wa kambi ya Magipsi ilioko Choisy-le-Roi, kusini mwa Paris, wanakaa ukingoni wa barabara.

Kabla ya hapo hadi sasa walikuwa wanaishi chini ya daraja ilioko katika barabara kuu, ndani ya magari yaliobadilishwa kuwa majumba na katika mahema karibu na barabara kuu ya A86. Hapo si mahala pazuri kwa mtu kujihisi yu nyumbani. Hivi sasa watu hao hawajuwi wapi watakapokwenda baadae "Hali yao itazidi kuwa mbaya. Hivi sasa hapa tuna watu 50 mabarabarani, wakiwa na watoto wadogo ambao, kwa sehemu, ni wagonjwa.

Hali ya usafi itazidi kuwa mbaya, kwa vile afisa mkuu wa serekali katika eneo hilo ametangaza kwamba hatakuwa tayari kuwapa makaazi watu hao." Hayo yamesemwa na Michel Fevre wa kutoka Chama cha Magipsi katika Ulaya. Hali hiyo inayowakuta Magipsi wa Choisy-le-Roi ndio vile vile inawakuta Magipsi wengi katika Ufaransa. Serekali imetangaza vita shidi yao. Malumbano hayo dhidi ya Magipsi ni sehemu ya mkakati mpya wa Rais Sarkozy wa kuleta usalama nchini Ufaransa. Kila muda makaazi yasiokuwa halali ya Magipsi huvunjwa.

Kuna karibu makaazi 600 ya aina hiyo nchini Ufaransa. Rais wa nchi hiyo ametangaza kwamba nusu ya makaazi hayo yawe yameshabomolewa ifikapo mwisho wa mwezi Oktoba. Kwa waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Hortefeux, yeye anaweza akajionea sura ya mwanzo ya zoezi hilo. Katika wiki mbili zilizopita, tumeyavunja makaazi 40 ya Magipsi. Hii inakupa sura ukubwa gani zoezi la kuwahamisha watu hao kutoka nchi litakavokuwa. Idadi ya watu hao ni karibu 700."

Magipsi ambao wameidanganya dola ya Ufaransa au kufanya uhalifu watarejeshwa makwao- hadi Rumania au Bulgaria. Ifikapo mwisho wa Agosti watasafisrihwa na ndege iliokodiwa na serekali ya Ufaransa. Wale ambao wataachiwa kubakia Ufaransa, kwa muda itawabidi watafute mahala pepya pa kupiga kambi. Labda hadi pale watakapofukuzwa nchini.

Kwa Michel Fevre, hali hiyo ni kwa makusudi kuwabadika sura mbaya watu hao. " Siasa hii haikubaliki. Waziri wa mambo ya ndani Hortefeux amewalenga Magipsi. na kila mara huwafungamanisah watu hao na uhalifu. Zaidi ni kwamba yeye sasa anawafukuza watu hao kutoka nchini, lakini yaonesha hatua hiyo haitatatua tatizo hilo."

Kwa Magipsi 15,000 walioko Ufaransa, kunaanza sasa kipindi kisiojulikana. Kambi zao nyingi nchini humo hazijapata kibali. Na pia sehemu ya upinzani, yaani kambi ya siasa za mrengo wa shoto, wanaunga mkono kuvunjwa makaazi hayo, kwa vile zinajuwa kwamba Wafaransa wengi wanaunga mkono kutokana na kuhofia kutoka michafuko.