1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahabusu 19 waokolewa Misri

Kalyango Siraj29 Septemba 2008

Wote wazima ila nusu ya watekaji 'waangamizwa'

https://p.dw.com/p/FR6C
Jangwa la Misri ambapo watalii 11 na wasaidizi wao walichukuliwa mateka.Picha: AP

Watalii wakizungu 11 pamoja na wamisri wanane waliochukuliwa mateka zaidi ya wiki moja iliopita katika jangwa nchini Misri wamekombolewa kwa msaada wa vikosi vya Usalama vya Misri na Sudan.Habari zaidi zasema kuwa baadhi ya wa watekaji wameuawa.

Kwa mujibu wa taarifa iliotolewa na shirika la habari la serikali ya Misri la Middle East News Agency-MENA mahabusi hao wote wameokolewa na wako salama salimini . Hata hivyo mazingira yaliyopelekea kukombolewa kwao baado hayajabainika. Lakini waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo Field Marshall Mohamed Hussein Tantawi amemuarifu rais Hosni Mubarak kuwa nusu ya watekaji nyara wameangamizwa.

Ameongeza kuwa hakuna pesa zote zilizotolewa kwa watekaji kama sharti la kuwaachilia huru mateka hao.

Habari za kuachiliwa huru watalii hao pamoja na wasaidizi wao wakiwemo na madereva zimethibitishwa na wizara ya mashauri ya kigeni ya Italy.

Lakini Ujerumani imesema baado inachunguza ukweli wa taarifa hizo. Msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni,Jens Ploetner amewashauri maripota kuzichukulia kwa tahadhari taarifa za kuachiliwa mateka.

Wajerumani tisa ni miongoni mwa mateka 19 wa Kizungu na Kimisri ambao walichukuliwa na genge la watu ambao walikuwa wamejifunika uso Septemba 19.Wengine ni raia watano wa Italy, raia mmoja wa Romania na raia wa Misri wanane. Wote hao walikamatwa katika sehemu za jangwa za magharibi mwa Misri.

Watekaji nyara walikuwa wamedai kulipwa dola zaidi ya millioni 8 na kuitaka Ujerumani ishughulikie malipo na pesa hizo zipewe mke wa mmoja wa walioanda safari ya watalii hao ambae naye ni miongoni mwa waliochukuliwa mateka.

Afisa mmoja wa Sudan amenukuliwa kusema kuwa mwanzo mahabusu hao walipelekwa katika eneo la milima linalozitenganisha Misri,Sudan na Libya kabla ya kupelekwa Chad.

Aidha Sudan inadai kuwa watekaji nyara hao ni wanachama wa kundi la waasi wa Darfur la Sudanese Liberational Army-Unity SLA-Unity.Lakini msemaji wa kundi hilo alikuwa amekanusha kuhusika ingawa alionya kuwa mahabusu wanaweza wakapata shida ikiwa nguvu zitatumiwa dhidi ya magaidi.

Afisa wa kiusalama wa Misri ambae hakutaka jina lake kutajwa,ameliambia shirika la habari la AFP kuwa vikosi maalum vya Misri vimewaokoa watalii hao baada ya operesheni iliofanywa ndani mwa Chad katika eneo linalokaribia mpaka wa Sudan.

Kuna taarifa kuwa jana jumapili vikosi vya Sudan viliwauwa watu sita ambao limewaita magaidi na kuwakamata wengine wawili baada ya kutupiana risasi katika eneo la mpaka wa Misri,Sudan na Libya.

Tukio la kuwateka nyara watalii limekuwa fedheha kwa serikali ya Misri ambapo utalii huchangia asili mia sita ya pato jumla la taifa.