1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama Kuu Kenya yawatia hatiani madaktari kwa mgomo

21 Desemba 2016

Mahakama Kuu nchini Kenya imewatia hatiani viongozi wa Chama cha Madaktari kwa kukiuka agizo la kusitisha mgomo ambao umekwamisha huduma za afya kote nchini kwa muda wa wiki tatu sasa.

https://p.dw.com/p/2UfRp
Kenia Ärzte Protest
Picha: Reuters/T. Mukoya

Akitoa uamuzi wake baada ya viongozi hao kufikishwa mahakamani, Jaji Hellen Wasilwa alisema maafisa wa Chama cha Madaktari walikuwa wanafahamu kwamba kulikuwa na agizo la mahakama lakini walikiuka. "Kwangu mimi kusema kwamba nastahili kutoa adhabu kwa kosa la kudharau mahakama si kwa ajili yangu kama jaji bali ni kwa ajili ya kuilinda sheria."

Jaji Wasilwa atatoa hukumu yake hapo kesho, huku kukiwa na wasiwasi kwamba huenda madaktari hao wanakabiliwa na tisho la kuwekwa gerezani kwa kukaidi agizo la mahakama.

Hata hivyo, madakatari wanasisitiza kwamba ni sharti makubaliano yaliyoafikiwa kati yao, serikali na Baraza la Magavana kuhusu nyongeza za mishahara yatekelezwe ndipo warejee kazini, huku magavana nao wakisema makubaliano hayo yanaweza tu kutekelezwa endapo madaktari watarudi kazini.

"Tuna uwezo wa kuzungumza na kukubaliana wakati tutakapoketi, lakini kwanza mrudi kazini, kwani kazi yenu inahusu maisha ya watu," alisema gavana wa Kiambu, William Kabogo.

Mvutano wa kisiasa waendelea

Protest in Kenia Raila Odinga 07.07.2014
Viongozi wa upinzani wa muungano wa CORD wanawatuhumu Jubilee kupanga kuiba kura, na wa Jubilee wanawashutumu CORD kwa shutuma hizo hizo.Picha: SIMON MAINA/AFP/Getty Images

Wakati huo huo, mvutano wa kisiasa kati ya upinzani na serikali bado unaendelea. Kikao maalum cha bunge kilichoitishwa na spika wa bunge la taifa kilivurugwa Jumanne (Disemba 20) na kuahirishwa hadi Alhamis wakati wabunge wangelikutana tena kujadili hoja ya kufanyia marekebisho sheria mpya ya uchaguzi.

Upinzani unapinga hatua ya kufanyiwa marekebisho sheria ya uchaguzi iliyopitishwa hivi majuzi kufuatia mapendekezo ya kamati iliyobuniwa kufanyia marekebisho mfumo wa uchaguzi, ukidai kwamba marekebisho ya sheria hiyo yalipendekezwa na Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC) na wala sio wabunge.

Kila upande, kati ya muungano wa Jubilee unaotawala na muungano wa CORD unaounda upinzani, unamlaumu mwengine kupanga njama za kuiba kura kwenye uchaguzi mkuu ujao hapo Agosti 2017.

Mwandishi: Alfred Kiti/DW Nairobi
Mhariri: Iddi Ssessanga