1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya Pakistan yasema zoezi la kumchagua Rais linaweza kuendelea kesho

Mohammed Abdul-Rahman5 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7iV
Rais Pervez Musharraf
Rais Pervez MusharrafPicha: AP

Mahakama kuu nchini Pakistan imeamua uchaguzi wa rais ambapo Rais Pervez Musharraf anatarajiwa kushinda, ujendelee kama ilivyopanga. Lakini imesema matokeo yasitangazwe hadi uamuzi utakapotolewa kuhusu uhalali wa Rais huyo.

Uamuzi wa mahakama kuu hii leo umekuja siku moja baada ya Jenerali Musharraf kufikia makubaliano na waziri mkuu wa zamani Benazir Bhutto wa kugawana madaraka baada ya uchaguzi wa bunge katikati ya mwezi Januari mwaka ujao. Hata hivyo mahakama inaweka wazi uwezekano wa kubatilisha matokeo ya uchaguzi rais, hadi kwanza uamuzi utakapotolewa kama akihitajika kwanza ajiuzulu kama mkuu wa majeshi au la .

Wadadisi wanasema kuahirisha uchaguzi kungeweza kuiingiza Pakistan katika vurugu zaidi za kisiasa Mahakama imepanga kikao kingine cha kusikiliza kisa hicho tarehe 17 ya mwezi huu. Mahakama ilikua inapitisha uamuzi leo kutokana na madai yaliowasilishwa na Makamu wa rais wa chama cha bibi Bhutto ,Makhdoom Amin Fahim na jaji mstaafu Wajihuddin Ahmad aliyekataa kula kiapo cha uaminifu baada ya Musharraf kutwaa madaraka kwa njia ya mapinduzi 1999.

Hatima ya Musharraf inafuatiliwa kwa makini,hasa na nchi za magharibi ambazo zina wanajeshi Afghanistan na wenye kuhisi wanakabiliwa na kitisho cha wanaharakati wa al-Qaeda wanaojificha katika mpaka wa Pakistan na Afghanistan.

Wakati huo huo kupatikana maafikiano juu ya kile kinachoitwa Upatanishi wa kitaifa utakaoweka msingi wa kuwepo mkataba wa kugawana madaraka baina ya Musharraf na Bibi Bhutto baada ya maafikiano ya hapo jana kati ya wajumbe wa pande hizo mbili, kulitarajiwa kuwekwa wazi hii leo.

Maafikiano hayo yanasemekana kuridhia dai la Bibi Bhutto kutaka vitisho na hatua za kuandamwa yeye na wanasiasa na maafisa wengine wa zamani wa serikali zisitishwe.Aidha mashitaka ya rushwa dhidi yake na wengine yatafutwa na kumuwezesha kurudi nyumbani tarehe 18 mwezi huu baada ya miaka zaidi ya minane ya kuwa uhamishoni, na hivyo kukiongoza chama chake cha Pakistan Peoples Party-PPP, kuelekea uchaguzi katikati ya mwezi Januari mwaka ujao.Jenerali Musharraf pia ameridhia takwa jengine la Bhutto, akisema atastaafu kama mkuu wa majeshi ifikapo tarehe 15 mwezi ujao wa Novemba.

Akizungumza mjini London, Bibi Bhutto aliyewahi kuwa Waziri mkuu mara mbili amesema ikiwa madai yake yatatekelezwa basi chama chake ambacho ni chama kikuu cha upinzani, hakitojiunga na vyama vyengine kujitoa bungeni na kuuhujumu uchaguzi wa rais hapo kesho. Wabunge wa chama hicho watajizuwia kupiga kura au watampigia kura mgombea wao. Muungano wa vyama vya upinzani unaoongozwa na chama cha waziri mkuu wa zamani Nawaz Shariff, utaususia uchaguzi huo.

Marekani kwa kutumia diplomasia ya kimya kimya, inasemekana imekua ikiwarai Musharraf na Bhutto washirikiane, ili kuizuwia Pakistan kuingia katika mikono ya wahafidhina wa kidini na kugeuka ngome ya wanaharakati wa msimamo mkali.