1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama yaamuru kuachiliwa kwa Hosni Mubarak

Admin.WagnerD21 Agosti 2013

Mahakama ya rufaa nchini Misri imeamuru Rais wa zamani wa nchi hiyo Hosni Mubarak kuachiwa huru,uamuzi ambao unabashiriwa kuligawanya hata zaidi taifa hilo huku umoja wa Ulaya ukikutana kuihusu Misri

https://p.dw.com/p/19UFl
Picha: picture-alliance/dpa

Mahakama ya Cairo imekubali ombi la wakili wa Mubarak la kuachiwa kwa kiongozi huyo aliyeiongoza Misri kwa miaka 30 kabla ya kung'olewa madarakani wakati wa wimbi la uasi lililoghubika mataifa mengi ya kiarabu mwaka 2011.

Wakili wake Farees al Deeb amethibitisha hilo baada ya kikao hicho cha mahakama kilichofanywa katika jela anakazouiliwa Mubarak la Tora.Alipoulizwa ni lini huenda Mubarak ataruhusiwa kuondoka gerezani, al Deeb alijibu pengine kesho.Haijabainika wazi hasa ni lini ataachiliwa.

Mubarak mwenye umri wa miaka 85 alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani mwaka jana kwa kushindwa kuepusha mauaji ya waandamanaji waliomng'oa madarakani lakini mahakama ilikubali rufaa yake mwaka huu na kuagiza kusikilizwa upya kwa kesi hiyo.

Wafuasi wa Rais aliyeng'olewa madarakani Mohammed Mursi
Wafuasi wa Rais aliyeng'olewa madarakani Mohammed MursiPicha: Reuters

Hata hivyo Mubarak bado anakabiliwa na mashitaka ya kutochukua hatua muafaka kuepusha mauaji hayo lakini tayari ameshakaa jela kwa kipindi kirefu zaidi kinachoruhusiwa kisheria kabla ya kuamuliwa kwa kesi na hivyo hakuna msingi wowote wa kuendelea kumzuilia.

Uamuzi hautapingwa

Mwendesha mashitaka Ahmed el Bahrawi amesema hatapinga uamuzi huo wa mahakama ya rufaa kwani mahakama hiyo ndiyo iliyo na maamuzi ya mwisho.

Mubarak anaonekana kutokuwa na mashiko tena katika siasa za Misi lakini kuachiliwa kwake kutachukuliwa na wamisri wengi kama kurejea kwa utawala unaosalimu kwa jeshi na wimbi la uasi la kutaka demokrasia lililomtoa madarakani kudunishwa na kuwa ubatili mtupu.

Hatua hiyo ya mahakama inawadia huku nchi hiyo ikijikuta katika mzozo wa kisiasa ambao umesababisha vifo vya zaidi ya watu 900 wakiwemo takriban maafisa 100 wa polisi na jeshi tangu kuondolewa madarakani kwa rais Mohammed Mursi wiki sita zilizopita.

Mawaziri wa mambo ya nje wa umoja wa Ulaya mjini Brussels wanakokutana kuihusu Misri
Mawaziri wa mambo ya nje wa umoja wa Ulaya mjini Brussels wanakokutana kuihusu MisriPicha: Georges Gobet/AFP/Getty Images

Jumuiya ya kimataifa imetiwa wasiwasi na ghasia za Misri na leo mchana mawaziri wa mambo ya nje wa umoja wa Ulaya wanakutana kujadili jinsi inaweza kutumia ushawishi wao wa misaada inayoipa Misri ya kima cha euro bilioni 6.7 kwa mwaka kuzilazimu pande zote katika mzozo huo kutafuta ufumbuzi wa mzozo huo na kusitisha ghasia.

Umoja wa ulaya wasitisha biashara ya silaha

Mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo Bi Catherine Ashton ametoa wito wa kutekelezwa kwa mchakato wa kisiasa utakaoirejesha Misri kwa njia ya kidemokrasia na kuongeza kuwa umoja huo umekuwa na mazungumzo na maafisa wa Misri kuhusiana hilo.

Marekani pia imesema inatathimini upya uhusiano wake na Misri na imesitisha zoezi la pamoja la mafunzo ya kijeshi huku ikitafakari kuhusu msaada wa mabilioni ya dola unayoipa Misi kila mwaka.

Nchi za kiarabu zenye utajiri mkubwa zikiongozwa na Saudi Arabia zimetangaza kuisadia Misri iwapo nchi za magharibi zitasitisha msaada wao na tayari Saudi Arabia,Kuwait na umoja wa falme za kiarabu umeahidi misaada ya dola bilioni bilioni 12 tangu Mursi kuondolewa madarakani.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/afp/dpa

Mhariri:Yusuf Saumu