1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama yathibitisha adhabu ya kifo kwa Mursi

Elizabeth Shoo16 Juni 2015

Mahakama moja ya Misri imethibitisha hukumu ya kifo kwa rais wa zamani Mohammed Mursi. Kiongozi huyo amekutwa na hatia ya kuhusika na mauaji ya mwaka 2011, wakati wa vuguvugu lililomwingiza madarakani.

https://p.dw.com/p/1Fi4h
Mohammed Mursi aliyekuwa rais wa Misri
Picha: Reuters/A. A. Dalsh

Mohammed Mursi, ambaye ni rais wa kwanza wa Misri kuchaguliwa kidemokrasia, alikuwa mahakamani akiisikiliza hukumu bila kusema chochote. "Mohammad Mohamed Mursi al-Ayat na Essam Mohamed Hussein el-Erian wanahukumiwa kifungo cha maisha kwa sababu ya uhalifu walioufanya."

Jaji Shaaban al-Shami aliisoma hukumu hiyo baada ya kushauriana na Mufti wa Misri. Kwa kawaida, maamuzi ya mufti si lazima yafuatwe na mahakama na hivyo hukumu ya leo itapelekwa pia kwenye mahakama kuu ya rufaa. Jaji al-Shami alithibitisha pia hukumu ya kifo kwa wanachama wengine watano wa Udugu wa Kiislamu, chama cha kisiasa cha Mursi ambacho sasa kimepigwa marufuku.

Mahakama imewakuta Mursi na wenzake na hatia ya kuua askari polisi watatu na kuwaachia huru wafungwa wapatao 20,000 suala lililozua ghasia kubwa katika maeneo ya mpaka kati ya Misri na Ukanda wa Gaza. Inaaminika kwamba wafungwa waliweza kuachiwa huru kwa sababu ya usaidizi kutoka kwa makundi ya wanamgambo wa kigeni.

"Pigo kwa demokrasia Misri"

Kabla ya hukumu ya kifo kusomwa, jaji al-Shami alimhukumu Mursi kifungo cha maisha jela, ambacho Misri ni sawa miaka 25. Hii ni kwa hatia ya kushirikiana na kundi la Kipalestina, Hamas. Wakati huo huo, kiongozi huyo wa zamani tayari yuko gerezani kwa kifungo cha miaka 20 alichohukumiwa kwa shutuma za kuhusika na mauaji ya mwaka 2012 ya waandamanaji, nje kasri lake, wakati alipokuwa bado rais.

Mohammed Mursi aliingia madarakani baada ya kung'olewa kwa Hosni Mubarak
Mohammed Mursi aliingia madarakani baada ya kung'olewa kwa Hosni MubarakPicha: picture-alliance/AP Photo/Khalil Hamra

Akiikosoa hukumu hiyo, Yehia Hamed aliyekuwa waziri wa uwekezaji nchini Misri na ambaye ni mwanachama wa Udugu wa Kiislamu alisema. "Tangazo la leo ni pigo jingine kwa demokrasia ya Misri," alisema Hamed. "Ni kilele cha karibu miaka miwili ya kumomonyoka kwa haki za binadamu tangu jeshi lilipoipindua serikali."

Aidha, Udugu wa Kiislamu umesema hukumu iliyotolewa ni batili na umetaka maandamano yafanyike Ijumaa ya wiki hii. Naye Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu amesema hukumu imechochewa kisiasa na kwamba haina misingi ya kisheria. Pamoja na hayo, Cavusoglu ameikosoa Misri kwa kukosa sheria na haki.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/ap/reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman