1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahasimu wa Kipalestina kuunda 'kamati ya maridhiano'

Bruce Amani
31 Julai 2023

Viongozi hasimu wa kisiasa wa Kipalestina Mahmud Abbas wa Fatah na Islmail Haniyeh wa Hamas waliokutana nchini Misri wameamua kuunda kamati ya maridhiano ya ndani ya Palestina.

https://p.dw.com/p/4UZUh
Ägypten Versöhungsgespräche mit der Hamas
Picha: Thaer Ganaim/apaimages/IMAGO

Hayo yalijiri wakati katika Ukanda Gaza, maelfu ya watu waliandamana kulalamikia tatizo lililokithiri la kukatika umeme na hali ngumu ya maisha, ikiwa ni ujumbe wa nadra wa wazi wa kutoridhishwa na serikali ya Hamas katika eneo hilo. 

Soma pia: Pande hasimu za Palestina zakutana Misri kutafuta suluhu

Rais Mahmud Abbas na kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh walikutana kwa mazungumzo ya nadra ya ana kwa ana katika mji wa pwani wa El Alamein nchini Misri pamoja na wawakilishi kutoka makundi ya kisiasa ya Kipalestina.

Jaribio hilo la karibuni la maridhiano linalenga kuziunganisha serikali mbili zinazoendeshwa sambamba za Hamas katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa na ile ya Mamlaka ya Palestina -- inayodhibitiwa na vuguvu la Fatah lake Abbas -- ambalo linatawala katika maeneo yanayoendeshwa na Palestina ya Ukingo wa Magharibi.

Marokko | Hamas Führer Ismail Haniyeh
Ismail Haniyeh ni mkuu wa kisiasa wa kundi la HamasPicha: AA/Stringer/picture alliance

Abbas na Haniyeh waliungana na wakuu wa makundi mengine, isipokuwa wa kundi lenye nguvu la Islamic Jihad na makundi mengine mawili madogo. Kwa mujibu wa washiriki wa mkutano huo, Haniyeh alitoa wito kwa Abbas kukomesha kile alichokiita ushirikiano wa usalama na Israel na kamatakamata za kisiasa.

Kiongozi huyo wa Hamas pia alisema bunge jipya, litakalojumuisha pande zote lazima liundwe kwa msingi wa uchaguzi wa kidemokrasia. Hamas ambayo ilishinda uchaguzi wa uliopita wa bunge katika mamlaka ya Palestina uliofanyika 2006, imekuwa ikiitisha kuandaliwa uchaguzi mkuu.

Akirejelea vurugu zilizozuka kati ya Hamas na Fatah baada ya kura hizo za 2006, Abbas mwenye umri wa miaka 87 amesema jana mapinduzi na mgawanyiko uliowakumba kwa miaka 17 lazima vikomeshwe. "Ninawaomba muunde kamati baina yenu kwa ajili ya kuendeleza mazungumzo kuhusu mambo mbalimbali yaliyojadiliwa leo ili kumaliza mgawanyiko na kufikia umoja wa kitaifa. Naiomba kamati hii ianze kazi mara moja ili kumaliza jukumu lake na kurudi kwetu na makubaliano au mapendekezo."

Abbas ameongeza kuwa lazima pande zote zirudi kwenye dola moja, mfumo mmoja, sheria moja na jeshi moja halali

Israelisch-palästinensischer Konflikt | Gaza
Wakaazi wa Gaza wanalalamikia ughali wa maishaPicha: Ali Jadallah/AA/picture alliance

Haniyeh ametoa wito wa kuundwa upya kwa Shirika la harakati za Ukombozi wa Palestina – PLO, taasisi inayokuza utaifa wa Palestina. PLO inajumuisha makundi mengi ya kisiasa ya Kipalestina lakini sio Hamas wala Islamic Jihad.

Mkutano wa jana ulijiri wakati ghasia zikizuka upya katika mzozo wa Israel na Palestina, hasa katika Ukingo wa Magharibi ambao Israel imeukalia tangu mwaka wa 1967.

Machafuko yaliyohusishwa na mgogoro huo mwaka huu yameuwaua karibu Wapalestina 203 na Waisrael 27 kwa mujibu wa takwimu za shirika la Habari la AFP.

Katika ukanda wa Gaza jana, maelfu ya watu waliandamana kulalamikia hali ngumu ya maisha na kuonyesha kutoridhishwa kwao na serikali ya Hamas inayoongoza katika Ukanda huo.

Hamasa inatawala Gaza kwa mkono wa chuma, na kuzuia maandamano na hata kukandamiza maramoja vitendo vya upinzani vinavyofanywa hadharani.

Na katika kambi kubwa kabisa ya wakimbizi wa Kipalestina nchini Lebanon, ya Ain al-Helweh katika mji wa bandari ya kusini wa Sidon, mapigano ya usiku kucha Jumapili yaliwauwa wanachama watano wa Fatah na mpiganaji mmoja wa itikadi kali.

AFP, AP