1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahasimu wagawana madaraka Zimbabwe

Kalyango Siraj15 Septemba 2008

Tsvangirai waziri mkuu na Mutambara naibu wake

https://p.dw.com/p/FIPo
Morgan Tsvangirai sasa waziri mkuu wa ZimbabwePicha: AP

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amekubali kugawana madaraka na mpinzani wake mkuu Morgen Tsvangirai.Duru za kuaminika zaeleza kuwa mpango huo unamuacha Mugabe kama rais huku mpinzani wake kama waziri mkuu.

Zimbabwe sasa imempata kiongozi mpya baada ya kipindi cha miaka 28.Kiongozi huyo ni Morgen Tsvangirai ambae sasa ni waziri mkuu wa nchi hiyo.

Hii imetokea baada ya rais Mugabe pamoja na Tsvangirai kutia sahihi mkataba rasmi wa kugawana madaraka.

Mtu wa kwanza kutangaza kuwa Tsvangirai ni waziri mkuu wa Zimbabwe alikuwa mpatanishi mkuu wa mgogoro huo na rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki.

Maelezo zaidi kuuhusu mpango huo baado ni finyu lakini madogo ambayo Deutsche Welle imeweza kuyapata yanaonyesha kuwa rais Mugabe atabaki kama rais wa nchi na kusimamia jeshi la ulinzi la nchi hiyo huku Morgen Tsvangirai ambae atakuwa waziri mkuu pia atasimamia jeshi la polisi.

Nae kiongozi wa tawi lililojitenga kutoka MDC Prof Arthur Mutambara atakuwa naibu waziri mkuu.

Duru ambazo zilikuwa karibu na mazungumzo ambayo yaliongozwa na rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini zinasema kuwa Tsvangirai kama waziri mkuu anatarajiwa kusimamia baraza la mawaziri ambalo linahusika na kuendesha masuala ya kila siku ya taifa hilo. Atasimamia mawaziri 31 ambao wamegawanywa kutoka vyama mbalimbali vya kisiasa nchini humo.

Katika hotuba yake ya kwanza kama waziri mkuu amewashukuru wale wote akiwemo Thabo Mbeki kwa juhudi zilizosaidia kufikia muafaka wa leo.

Taarifa zaidi zasema kuwa chama cha Mugabe cha ZANU PF kitatoa mawaziri 15,chama cha Tvangirai cha MDC kitoe mawaziri 13 halafu chama cha MDC cha Mutambara ambacho ni cha upinzani mdogo kitatoa mawaziri watatu.

Rais Mugabe ambae ametawala nchi hiyo tangu mwaka wa 1980 amekubali kugawana baadhi ya madaraka yake.

Sherehe ya leo imeshuhudiwa na viongozi mbalimbali kama vile mfalme Muswati wa Swaziland akiwa kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya jumuia ya mataifa ya kusini mwa Afrika ya SADC, rais Jakaya Kikwete wa Tanzania kama mwenyekiti wa Umoja wa Afrika pamoja na mptanishi mkuu wa SADC na mwenyekiti wa jumuia hiyo rais Thabo Mbeki.

Tsvangirai ameungwa mkono na baadhi viongozi wa Afrika,mkiwemo rais wa Botswana Ian Khama na waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema mpango huo, wa kugawana madaraka,ni tete mno na utahitaji mahasimu hao wa zamani kuweka kando tofauti zao washirikiane ili kutoa shaka miongoni mwa walio na shaka hizo kama vile mataifa ya magharibi ambayo yatachangia sana katika ukarabati kwa kutoa fedha za kusaidia kazi hiyo.