1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahujaji wa Kiislam leo waanza ibada ya hija Saudi Arabia

17 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CcTB

MECCA

Zaidi ya mahujaji wa Kiislam milioni moja na laki sita kutoka duniani kote leo wanaanza ibada ya hija nchini Saudi Arabia ikiwa ni siku ya nane ya Dhi al Hajj kwa mujibu wa kalenda ya mwezi.

Mamia kwa maelfu ya wananchi wa Saudia Arabia halikadhalika wageni wanaoishi nchini humo pia wanatazamiwa kushiriki ibada hiyo.

Waislamu wote wanatakiwa kufanya ibada hiyo ya hijja mjini Mecca angalau mara moja katika umri wa maisha yao ikiwa wana uwezo na afya.Miongoni mwa mahujaji wa mwaka huu ni Rais Mahmoud Ahmedinejad wa Iran ambaye amealikwa na Mfalme Abdullah wa Saudia Arabia na anakuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran kushiriki ibada hiyo.

Saudi Arabia imetangaza kwamba kipengele kikuu cha ibada hiyo wakati mahujaji watakapokusanyika kwenye Mlima Arafa karibu na Mecca kitatekelezwa hapo kesho Jumanne.

Siku inayofuata hapo Jumaatano itakuwa siku ya Eid la Adha sherehe ya kuchinja ambapo Waislamu huchinja kondoo au mbuzi kuadhimisha kumalizika kwa ibada hiyo ya Hijja.

Takriban wanyama milioni mbili huchinjwa wakati wa kila ibada ya hija kuadhimisha tendo la Nabii Ibrahim kuwa tayari kumtolea muhanga mwanawe wa kiume Ismail kwa ajili ya Mwenyeenzi Mungu.