1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahusiano kati ya Marekani na Saudi Arabia mashakani?

29 Septemba 2016

Wataalamu wameonya Saudi Arabia huenda ikapunguza ushirikiano muhimu na mshirika wake wa muda mrefu Marekani. Bunge la Marekani limewaruhusu wahanga wa mashambulizi ya Septemba 11, 2001 kuushitaki ufalme huo.

https://p.dw.com/p/2QkBz
USA Washington Senatoren John Cornyn und Chuck Schumer
Picha: Getty Images/D. Angerer

Kukata ushirikiano ni miongoni mwa mambo ambayo Saudi Arabia inaweza kuyafanya baada ya bunge la Marekani, Congress, kupiga kura siku ya Jumatato wiki hii kubatilisha kura ya turufu ya rais Barack Obama kuzuia sheria ya Haki dhidi ya wafadhili wa ugaidi, kifupi JASTA.

Mabaraza yote mawili ya bunge la Marekani, baraza la seneti na baraza la wawakilishi, yalipiga kura Jumatano wiki hii kupitisha sheria hiyo ambayo itaziruhusu familia za wale waliokufa katika mashambulizi ya mwaka 2001 mjini New York kudai fidia kutoka kwa serikali ya Saudi Arabia. 

Saudi Arabia imekuwa ikipinga kila mara shaka shaka zilizopo kwamba iliwafadhili washambuliaji, waliowaua watu karibu 3,000 chini ya mwavuli wa kundi la wanamgambo wa kiislamu la al Qaeda. Washambuliaji 15 kati ya 19 walioziteka nyara ndege za abiria na kuzitumia katika mashambulizi ya Septemba 11 walikuwa raia wa Saudi Arabia. 

World Trade Center New York Ground Zero
Jengo la shirika la biashara la kimataifa liliposhambuliwa New YorkPicha: Reuters

Serikali ya Saudi Arabia ilidhamini kampeni kubwa ya ushawishi dhidi ya sheria ya JASTA kabla kura iliyopigwa bungeni, na kuonya ingehujumu kanuni ya ulinzi wa taifa huru. Hata hivyo maafisa wa ufalme huo walisita kutishia hatua watakazozichukua iwapo sheria hiyo ingepitishwa. Ushirika wa muda mrefu kati ya ufalme wa Saudi Arabia na Marekani ni mojawapo ya nguzo muhimu za siasa za Mashariki ya Kati, usalama na biashara, na katika kauli zao siku ya Alhamisi raia kadhaa wa Saudia walisema sheria ya JASTA ingehatarisha kile wanachokiona kama uhusiano wa kutegemeana.

"Nini kitakachotokea kama Saudia Arabia itasitisha ushirikiano wake na Marekani katika mapambano dhidi ya ugaidi kama hatua ya kujibu kupitishwa kwa sheria ya JASTA?" aliandika Salma al-Dosary, mhariri mkuu wa gazeti la Al Sharq al-Awsat, linalomilikiwa na Saudi Arabia, katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.

Raia mwingine wa Saudia aligusia kuhusu imani pana ya muda mrefu katika eneo hilo kwamba Marekani inautaka utajiri wa mafuta wa ufalme huo. "Sheria ya JASTA ni fursa ya mwisho kwa Marekani kuzikamua raslimali za taifa letu zuri," akaandika Abdullah Medallah katika Twitter.

Baadhi ya wachambuzi wanahoji kwamba familia ya Al Saud itaichukulia hatua ya kupitishwa sheria hiyo kama ya masilahi ya kisiasa kwa wabunge katika kipindi cha uchaguzi nchini Marekani na kwamba uwezekano wa kesi yoyote dhidi ya ufalme wa Saudi Arabia kufaulu haujulikani. Hata hivyo sheria hiyo haifanyi chochote katika kuondosha msuguano wa muda mrefu kati ya Marekani na Saudi Arabia.

USA Gedenken Anschläge vom 11. September 2001
Rais Obama, kulia, na waziri wa ulinzi wa Marekani, Leon Panetta, wakiongoza kumbukumbu za miaka 11 ya mashambulizi ya Septemba 11Picha: Reuters

Rais Obama, ambaye alitumia kura yake ya veto kuizuia sheria ya JASTA lakini akazidiwa nguvu na bunge la Marekani, anaendelea kuonekana na ufalme wa Saudi Arabia na mataifa jirani ya eneo la Ghuba akilipendelea taifa hasimu mkubwa Iran, madai ambayo utawala wa mjini Washington unayapinga. Obama pia anaonekana anatofautiana na serikali ya mjini Riyadh kuhusu suala la Syria na mizozo mingine katika mataifa ya kiarabu.

Mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Falme za Kiarabu, UAE, Abdulkhaleq Abdulla, amesema, "Sheria hii inadhihirisha kampeni dhidi ya Saudi Arabia. Ni wakati wa kuona Amerika kidogo katikati yetu."

Baadhi ya wachambuzi wamebashiri kwamba Riyadh huenda ikajibu kwa kuzuia biashara ya Marekani na taifa hilo lenye uchumi mkubwa Uarabuni au kuuwekea mipaka ushirikiano katika masuala ya usalama, mapambano dhidi ya ugaidi na juhudi za kutafuta amani katika mizozo ya nchi za kiarabu. 

Mchanganuzi wa masuala ya siasa Theodore Karasik wa Taasisi ya Gulf State Analytics aliandika katika tovuti ya al Arabiya kwamba sheria ya JASTA "itachochea wimbi la malumbano makali ya kisheria yatakayofuja moja kwa moja mahusiano ya kisiasa katika wakati ambapo ushirikiano imara katika mapambano dhidi ya ugaidi unahitajika."

Mwandishi: Josephat Charo/rtre/afpe
Mhariri: Mohammed Khelef