1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mainz iko kileleni mwa Bundesliga

20 Septemba 2010

Mabao 3 ya Berbatov yahakikisha ushindi wa Manchester United dhidi ya Liverpool.

https://p.dw.com/p/PHbQ
Magath na Raul hawakufua dafu mbele ya B.Dortmund (3:1)Picha: AP

LIGI ZA ULAYA:

Katika Bundesliga,mainz imeparamia kileleni mwa Bundesliga wakati katika Serie A-Ligi ya itali Mabao ya Samuel Eto'o yaitimua Palermo nje kwa mabao 2:1.

Dimitry Berbatov aipatia Manchester united mabao 3 pekee na kuizima Liverpool kwa 3-2 .nae Cristiano Ronaldo apigwa mkwaju maridadi kuipa ushindi Real Madrid wa m,abao 2-1 dhidi ya Real Sociedad.

Katika Kom,be la klabu bingwa barani Afrika Esperence yaipiga kumbo Dynamos ya Zimbabwe kwa bao 1:0.Na Simba ya Tanzania, yashindwa kunguruma mbele ya Polisi katika Ligi ya Taifa.

"Michezo Mwishoni mwa Wiki":

Katika Bundesliga, Mainz ndio ilioparamia kileleni mwa Bundesliga baada ya kuichapa werder bremen jumamosi mabao 2:0 kama vile Mounira Mohammed anavyosimulia:

Mainz, inaongoza kwahivyo Bundesliga kwa msangao wa mashabiki wengi ikiwa na pointi 12 kutoka mapambano 4 ya kwanza ya msimu huu.Ushindi wa mabao 2:0 dhidi ya Bremen,utaiweka Mainz, kileleni kwani kesho Jumaane, watatamba nyumbani dhidi ya FC Cologne, iliomudu suluhu 0:0 na mabingwa Bayern Munich .

Munich, imeangukia nafasi ya 9 ya ngazi ya Ligi.Munich haikutia bao tangu mpambano wao wa kwanza kabisa msimu huu hapo august 20 na msukosuko unaendelea kama ulivyowaandama wenzao makamo-bingwa Schalke.

Schalke ndio inayoburura hivi sasa mkia wa Bundesliga.Licha ya kuwaajiri mastadi kadhaa miongoni mwao Raul kutoka Real Madrid,Spain, alikoichezea klabu hiyo kwa miaka 17,Schalke ililazwa kwa mabao 3:1 na maahasimu wao wa mtaani Dortmund.

Firimbi ya mwisho ilipolia na Schalke kujikuta hoi, haina hata pointi 1 tangu kuanza msimu,kocha wao Felix Magath , aliepata umaarufu alipoitawaza Wolfsburg mwaka juzi mabingwa na Schalke makamo- bingwa mwaka jana alisema:

"Inanisikitisha sana kwa mashabiki wetu ambao waliweka matarajio makubwa kama sisi.Kwa bahati mbaya , leo kwa mara ya kwanza timu yetu imecheza kwa hofu na wasi wasi mkubwa na haikuweza kabisa kutoa changamoto kwa adui."

Ama katika Premier League, Dimitar Berbatov, alipiga hodi mara 3 katika lango la Liverpool na kuitikiwa "karibu ndani" na hivyo ,akaipa ushindi Manchester United wa mabao 3-2.

Chelsea, mabingwa, waliendelea kutamba na kuondoka na ushindi wao wa 5 msimu huu wakiwa wametia jumla ya mabao 21.Chelsea, iliitandika Blackpool mabao 4:0 .

Mabao yote ya Chelsea, yalitiwa wavuni kipindi cha kwanza kwa Florent Malouda akitia mabao 2 na Didier Drogba na mwenzake wa Corte D'iviore , Salomon Kalou.

Chelsea, inaongoza Premier League ikiwa na pointi 15 kileleni,pointi 4 mbele ya Manu na Arsenal iliomudu suluhu tu ya bao 1:1 na Sunderland.Manchester city ilijongea hadi nafasi ya 4 ya ngazi ya Ligi kwa kutandika Wigan Athletic 2-0.

Katika la Liga-Ligi ya Spain, Cristiano Ronaldo, alilifumania lango la Real Sociedad kwa mkwaju maridadi mnamo dakika ya 74 ya mchezo.Real Madrid, iliondoka na ushindi 2:1.

Mabingwa FCBarcelona , wamerudi kutamba pale muargentina ,Lionel Messi na Gerald Pique, walipoitikiwa hadi zao langoni mwa lango la Atletico Madrid na kutwaa ushindi wa mabao 2-1.Ushindi wao huo, ulitiwa dosari na kuumia goti kwa stadi wao Lionel Messi.

Katika Serie A,Ligi ya itali, mabingwa wa ulaya Inter Milan, wanaongoza Ligi hiyo pamoja na Cesena, iliopanda daraja ya kwanza msimu huu baada ya kupita mapambano 3 ya kwanza . Inter Milan ,iliotwaa vikombe 3 msimu uliopita, viwili nyumbani na Champions League, barani Ulaya, ilihitaji mabao 2 ya Mkameroun, Samuel Eto.o, kuzima vishindo vya Palermo. Inter, ilishinda kwa mabao 2:1. Sampdoria ingeweza kugawana uongozi wa Ligi laiti ingeshinda,lakini ilizabwa mabao 2:1 na Napoli.

Katika kinyan'ganyiro cha kuania tiketi ya nusu-finali ya kombe la klabu bingwa barani Afrika, kama ilivyotazamiwa Esperence ya Tunisia imeitimua nje Dynamo ya Zimbabwe, mjini Harare,kwa bao 1:0.

Jose Mourinho,kocha wa Real Madrid, alieitawaza Inter Milan, mabingwa wa ulaya,hataridhia kuwa kocha wa timu ya Taifa lake Ureno, ili kuiongoza kwa muda katika kinyan'ganyiro cha kuania kufuzu kwa Kombe lijalo la Ulaya 2012. Mourinho,aliombwa na shirikisho la dimba la Ureno kuwa kwanza asimamie mpambano kati ya Ureno na Denmark n yumbani hapo Oktoba 8 na baadae ule na Iceland siku4 baadae.

Kocha huyo wa Real Madrid, aliwaambia maripota mwishoni mwa wiki kuwa, hawezi kuitikia ombi la Ureno ,kwavile, aliamini kwamba, timu yake ya Real isingefurahia kuondoka kwake kuishughulikia timu hiyo ya Taifa.

Ureno, ilimtimua kocha wake Carlos Quiroz, mwezi huu kufuatia kusimamishwa kazi kwa miezi 6 kwa kuwatukana wachunguzi wa madhambi ya (doping ) kabla kuanza kwa Kombe lililopita la dunia .Bado Ureno, haikumpata kocha mpya kujaza pengo lake wakati inaania tiketi yake ya kufuzu kwa Kombe la Ulaya la Mataifa, 2012 litakaloaniwa Poland na Ukraine kwa ubia.

Mwandishi: Ramadhan Ali/ TRE/AFPE/DPAE

Mhariri:Abdul-Rahman