1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maiti ya Gaddafi kuzikwa leo

21 Oktoba 2011

Maiti ya aliyekuwa kiongozi wa Libya, kanali Muammar Gaddafi itazikwa leo, huku viongozi wa baraza la mpito la nchi hiyo wakijiandaa kutangaza kukombolewa kwa umma wa Libya kutoka utawala wa mkono wa chuma wa Gaddafi.

https://p.dw.com/p/12wOJ
Muammar Gaddafi wakati wa uhai wakePicha: picture-alliance/dpa

Baraza la mpito la Libya litatangaza rasmi ukombozi kamili wa nchi hapo kesho kufuatia kifo cha kanali Muammar Gadafi. Waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Libya, Mohmoud Jibril, amesema wananchi wa Libya wanapaswa kufahamu kwamba enzi mpya imeanza nchini mwao baada ya Gaddafi kuuwawa.

"Huu ni wakati wa kuijenga Libya mpya na uchumi mpya, mfumo mpya wa elimu na mfumo mpya wa afya. Ni wasaa wa kuwa na mtizamo mpya wa mustakabali wa wananchi wa Libya."

Ripoti ya uchunguzi wa daktari

Akiinukulu ripoti ya uchunguzi wa daktari, Jibril alisema Gaddafi alikufa kutokana na jeraha la risasi kichwani alilolipata wakati wa ufyetulianaji wa risasi kati ya wapiganaji wa serikali na wafuasi wake, baada ya kukamatwa katika mji alikozaliwa wa Sirte.

Mahmud Dschibril / Libyen / Übergangsrat
Waziri mkuu wa baraza la mpito la Libya, Mahmoud JibrilPicha: dapd

Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limetaka kifo cha Gaddafi kichunguzwe. Msemaji wa majeshi ya baraza la mpito la Liba, Amhed Bani amesema:

"Gaddafi alikamatwa wakati alipokuwa amejificha. Alipinga kukamatwa na akauwawa kama mtu mwingine yeyote anayekuwa kitisho. Sidhani ulimwengu utatubeza kwa hilo. Muhimu ni kwamba Gaddafi amekufa."

Taarifa za kutatanisha

Taarifa za kutatanisha zimejitokeza kuhusu jinsi Gaddafi alivyokufa baada ya kukamatwa, kufuatia shambulio la anga lililofanywa na jumuiya ya kujihami ya NATO dhidi ya msafara wake, wakati ulipojaribu kuondoka mji wa Sirte uliokuwa umezingirwa.

Taarifa ya daktari aliyeifanyia uchunguzi maiti ya Gaddafi imesema kiongozi huyo alitolewa kutoka bomba la majitaka na hakuonyesha upinzani wowote. Wapiganaji walipoanza kumhamisha, alipigwa risasi mkono wake wa kuume na walipomuweka kwenye gari hakuwa na majeraha mengine. Lakini gari hilo lilipokuwa likienda, kukatokea ufyetulianaji wa risasi kati ya wapiganaji wa mapinduzi na vikosi vya Gaddafi, ambapo alipigwa risasi kichwani. Daktari huyo hakuweza kubaini ikiwa risasi hiyo ilitoka upande wa wapiganaji wa baraza la mpito au vikosi vya Gaddafi.

Gaddafi alikuwa hai alipochukuliwa kutoka Sirte, lakini akafa dakika chache kabla kufika hospitalini. Sampuli ya dumu na chembechembe za urathi zilichukuliwa kutoka kwa maiti yake pamoja na nywele, lakini ikabainika nywele zake zilikuwa bandia, hivyo kuthibitisha tetesi zilizokuwa zimezagaa kwamba Gaddafi alikuwa amefanyiwa operesheni kuwekewa nywele bandia.

Lakini kwa mujibu wa kamanda wa vikosi vya wapiganaji wa baraza la mpito, Mohammed Leith, Gaddafi alikuwa kwenye gari aina ya Jeep wakati walipoanza kuifyetulia risasi. Alishuka na kujaribu kukimbia na kujificha kwenye bomba la maji taka. Wapiganaji wakafyetua tena risasi na akatoka akiwa ameshika bunduki aina ya Kalashnikov mkononi na bastola ya dhahabu kwenye mkono mwingine. Alitazama kushoto na kulia na kuuliza kilichokuwa kikiendelea. Wapiganaji wakafyetua risasi na kumjeruhi mguu na bega lake. Baadaye akafa.

Harakati ya NATO yafika kikomo

Frankreich Außenminister Alain Juppe
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Alain JuppePicha: dapd

Kwa upande mwingine waziri wa mashauri ya kigeni wa Ufaransa, Alain Juppe, amesema leo kwamba nchi yake inazichukulia harakati za kijeshi za jumuiya ya kujihami ya NATO nchini Libya kuwa zimefika kikomo, kufuatia kuuwawa kwa Gaddafi. Viongozi wa jumuiya ya NATO wanakutana baadaye leo mjini Brussels, Ubelgiji kujadili kumaliza operesheni yao iliyodumu miezi saba nchini Libya.

Gaddafi kuzikwa leo

Maiti ya Gaddafi imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika eneof la zamani la soko mjini Misrata. Maziko mafupi na ya haraka haraka yanatarajiwa kufanyika baadaye leo katika mahala pa siri, kufuatia taratibu za dini ya kiislaumu

Gaddafi kuzikwa leo

Maiti ya Gaddafi imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika eneof la zamani la soko mjini Misrata. Maziko mafupi na ya haraka haraka yanatarajiwa kufanyika baadaye leo katika mahala pa siri, kufuatia taratibu za dini ya kiislaumu

Mwandishi: Josephat Charo/

Mhariri: Yusuf Saumu