1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majadiliano kujumuisha wahamiaji Ujerumani

B.Günghör - (P.Martin)7 Novemba 2008

Hata mkutano wa kilele wa tatu kujumuisha jamii za kigeni zinazoishi nchini Ujerumani,haukuweza kutekeleza malengo yake.

https://p.dw.com/p/Fp9V

Mara nyingine tena serikali na wajumbe wa wakazi wanaoihisi kuwa wanastahmiliwa Ujerumani,badala ya kutambuliwa kama wakazi wenzao wenye haki sawa sawa,hawakuweza kuondosha tofauti za maoni kati ya pande hizo mbili.

Haitokuwa haki kupaza sauti na kuilaumu serikali ya sasa ya Ujerumani, kwani makosa yalifanywa tangu wakati wa utawala wa serikali kuu zilizotangulia na hata serikali za mikoani.Bila shaka Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na mjumbe wake maalum anaeshughulikia masuala ya kujumuisha wahamiaji katika jamii za Kijerumani,Maria Böhmer wanastahili kusifiwa kwani wao ndio wanahimiza majadiliano ya moja kwa moja pamoja na wajumbe wa wahamiaji nchini Ujerumani.

Lakini haitoshi kuwa na azma tu,kwani hali iliyokuwepo yapaswa kutambuliwa ili malengo yaliyowekwa yaweze kutimizwa.Muhimu kabisa ni kutambua kuwa Mradi wa Kitaifa wa mwaka mmoja wenye azma ya kuwajumuisha wahamiaji katika jamii za Kijerumani ulio na kama mapendekezo 400 kutoka pande zote mbili,haujaleta mabadiliko yaliyotazamiwa na itachukua muda mrefu kufikia malengo hayo.Jamii haziwezi kujumuishwa kwa amri ya serikali.Kinachohitajiwa ni kwa pande zote mbili kuwa na lengo moja ili ziweze kuishi bila ya mivutano licha ya tofauti za kidini na kitamaduni. Mito ya kuwa na baraza maalum litakalokutana mara kwa mara kujadiliana na kushauriana juu ya masuala ya jamii iliyojumuika si tataizo kwa Kansela Merkel.Yeye anaunga mkono majadiliano yenye mpango.

Ujerumani wanaishi watu milioni 15 wenye asili za kigeni,nusu yao wakiwa na uraia wa Kijerumani.Idadi ya raia wasiotambulika barabarani kama wageni na waliofanikiwa katika sekta ya uchumi na kujumuika katika jamii za Kijerumani,ni kubwa zaidi kuliko kundi ambalo halikujijumuisha na hutazamwa kama ni tatizo.Kwa maoni ya mbunge wa chama cha SPD Lale Akgün alie na asili ya Kituruki,watu wote wanaoishi Ujerumani na kuheshimu sheria za nchi na hulipa kodi zao,wachukuliwe kama wakazi waliojijumuisha bila ya kujali husikiliza muziki wa aina gani majumbani mwao au husoma magazeti gani.