1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majadiliano pamoja na Hamas ndio njia ya kumaliza mapambano

S.Engelbrecht / P.Martin29 Februari 2008

Israel ikijikuta katika mzunguko wa mashambulizi tangu kufunga mpaka wake na Ukanda wa Gaza,mwanaharakati wa Kiisraeli anaegombea amani,Uri Avnery anasema chama cha Hamas kisingepinga pendekezo la kuwa na majadiliano.

https://p.dw.com/p/DFg7
Uri Avnery.jpg Uri Avnery, winner of the Alternative Nobel in 2001 speaks during the opening of a six-day seminar on the 25th anniversary of Right Livelihood Awards, in Salzburg, Austria, Wednesday, June 8, 2005. The award was created by Swedish-German stamp collector Jakob von Uexkull in 1980. (AP Photo/Martin Schalk)
Mwanaharakati wa Kiisraeli,Uri AvneryPicha: AP

Waisraeli na Wapalestina wanahesabu wafu wao. Makombora aina ya Kassam yanayorushwa na Wapalestina yanaua na kujeruhi wakaazi katika miji ya Sderot na Aschkelon kusini mwa Israel;na roketi za Israeli pia zinaua wanamgambo wa Hamas-na mara nyingi,wahanga ni raia wa Kipalestina wamaoishi Ukanda wa Gaza.Yadhihirika kuwa katika mgogoro wa Israel na Hamas hakuna dalili ya kupunguka kwa hali ya mvutano.

Siku ya Alkhamisi,hadi Wapalestina 20 waliuawa baada ya ndege za kijeshi za Israel kushambulia Ukanda wa Gaza kujibu mashambulizi mapya ya wanamgambo wa Hamas waliyorusha roketi kusini mwa Israel hapo siku ya Jumatano na kusababisha kifo cha Muisrali mmoja katika mji wa Sderot.Kwa mujibu wa Hamas,wanamgambo wa Kipalestina tangu Jumatano wamevurumisha hadi makombora 81 kusini mwa Israel.Si chini ya Wapalestina 32 wameuawa kwenye Ukanda wa Gaza katika mashambulizi ya siku mbili yaliyofanywa na ndege za Israel.

Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert anadhamiria kuendelea na mashambulizi ya anga na kulitenga eneo la Gaza ili kuhakikisha usalama wa wananchi wake.Kwa maoni ya mwanaharakati wa Kiisrael Uri Avnery hiyo si sawa. Anasema:

O -TON AVNERY:

"Juhudi zote za kutaka kuwateketeza Hamas kwa njia za kijeshi;kuwaua wanasiasa na viongozi wao wa kijeshi: kuvamia na kukalia eneo zima la Ukanda wa Gaza - yote hayo hayatosaidia.Historia inatuambia kuwa hatua za aina hiyo haziwezi kuteketeza makundi kama vile Hamas;badala yake hujakuwa maarufu zaidi."

Lakini Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert ana maoni tofauti kabisa.Yeye amesema,nchi yake itaendelea kuwashambulia Wapalestina kwenye Ukanda wa Gaza mpaka hali ya usalama itakaporejea kwa wakaazi wa kusini mwa Israel. Lakini mwanaharakati Uri Avnery anasema,Olmert anangángánia zaidi itikadi zake.Kwa maoni yake wanasiasa kama vile waziri mkuu wa Israel,anapaswa kuamua lipi lililo muhimu zaidi:-kubakia muaminifu kwa itikadi zake za kisiasa au kukomesha umwagaji damu.

Mwanaharakati huyo mwenye umri wa miaka 84 anasema,chama cha Hamas katika siku za nyuma mara kadhaa kiliwahi kusema kuwa kipo tayari kujadiliana kuweka chini silaha lakini pendekezo hilo limekataliwa na serikali ya Israel.Msimamo wa rasmi wa Hamas ni kuwa Rais wa Wapalestina Mahmud Abbas anaweza kujadiliana na Israel iwapo anataka kufanya hivyo.Lakini makubaliano yatakayopatikana lazima yaridhiwe na umma wa Palestina. Kwa maoni ya Avnery na kundi lake la "Gusch Schalom" linalogombea amani,majadiliano pamoja na Hamas ndio njia ya kumaliza mapambano.Kufuatia mashambulizi ya makombora ya miaka saba,sasa kama theluthi mbili ya Waisraeli wanaunga mkono majadiliano pamoja na Hamas.Uchunguzi wa maoni uliofanywa na gazeti la Kiisraeli "Haáretz" umeonyesha kuwa asilimia 64 ya umma unaunga mkono majadiliano pamoja na Hamas.