1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majadiliano ya amani yagubikwa na suala la makaazi

14 Septemba 2010

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas hii leo wamekutana kwa majadiliano ya ana kwa ana katika mji wa Sharm-el-Sheikh nchini Misri. .

https://p.dw.com/p/PC4s
US Secretary of State Hillary Rodham Clinton, center, meets with Israeli Prime Minister Benjamin Netanyahu, left, and Palestinian President Mahmoud Abbas in Sharm El-Sheikh, Egypt Tuesday, Sept. 14, 2010. Clinton is in the region for Mideast peace talks.(AP Photo/Alex Brandon, Pool)
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton(kati) akikutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu(kushoto) na Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas katika mji wa Sharm-el-Sheikh Misri.Picha: AP

Lakini majadiliano hayo ya amani yaliyofanywa chini ya uongozi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton, yamegubikwa na mzozo unaohusika na makaazi ya walowezi wa Kiyahudi.

Wapalestina na Waisraeli waliokutana Sharm-el-Sheikh hawakuonyesha dalili za kuafikiana kuhusu suala tete la ujenzi wa makaazi ya Wayahudi katika ardhi iliyokaliwa na Waisraeli kwenye Ukingo wa Magharibi. Wapalestina wanataka eneo hilo kuwa sehemu ya taifa lao jipya litakaloundwa katika siku zijazo.

Mpatanishi wa Wapalestina, Nabil Shaath amesema, wanajaribu kumfahamisha Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu kuwa makaazi hayo ni suala muhimu sana kwa majadiliano ya amani. Majadiliano hayawezi kufanywa wakati Israel ikiendelea kujiimarisha katika maeneo iliyoyakalia.

Jumapili iliyopita, Netanyahu alisema kuwa hatorefusha muda wa kusitisha sehemu ya ujenzi wa makaazi ya Wayahudi,kipindi hicho kitakapomalizika Septemba 26. Akaashiria kuwa atadhibiti kiwango cha ujenzi wa makaazi hayo.

Lakini, Wapalestina wametishia kujitoa kwenye majadiliano ya ana kwa ana ikiwa ujenzi huo utaanzishwa upya.

Waziri Clinton aliekutana na Waziri Mkuu Netanyahu na Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas, amesema pande zote mbili zinapaswa kuchukua hatua za kuumaliza mzozo huo. Wakati huo huo, mjumbe maalum wa Marekani katika Mashariki ya Kati George Mitchell akieleza msimamo wa Washington kuhusu suala hilo tete amesema:

" Kama Rais Obama alivyosema hivi karibuni, tunaamini kuwa inaingia akilini kurefusha muda wa kuzuia ujenzi wa makaazi hayo, hasa majadiliano yakionyesha kuendelea vizuri."

Serikali ya Marekani imepanga kupata mfumo wa makubaliano ya amani katika kipindi cha mwaka mmoja. Mfumo huo utazingatia masuala muhimu. Miongoni mwao ni makaazi ya walowezi wa Kiyahudi, usalama, mipaka na hatima ya wakimbizi wa Kipalestina.

Kesho Jumatano, Clinton atakutana tena na Netanyahu na Abbas mjini Jerusalem katika jitahada ya kuendeleza mazungumzo hayo ya ana kwa ana. Siku ya Alkhamisi anatazamia kuonana na Waziri Mkuu wa Wapalestina Salam Fayyad mjini Ramallah kabla ya kuelekea Amman na kuikamilisha ziara yake kwa kukutana na Mfalme Abdallah wa Jordan.

Mwandishi:Martin,Prema/DPAE/RTRE

Mpitiaji: M.Abdul-Rahman