1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majanga yaongezeka duniani

Josephat Charo15 Desemba 2006

Wajerumani walitoa mchango mkubwa zaidi mwaka wa 2005 kukabiliana na majanga asili. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti kuhusu majanga asili iliyowasilishwa mjini Berlin na rais wa chama cha msalaba mwekundu nchini Ujerumani, Rudolf Seiters. Ripoti hiyo imezungumzia pia jukumu la vyombo vya habari katika kuripoti majanga duniani.

https://p.dw.com/p/CHlt
Majanga asili yaongezeka duniani
Majanga asili yaongezeka dunianiPicha: AP

Tatizo linapozungumziwa huwa limetatuliwa nusu. Waathiriwa wengi wa majanga asili huwachwa bila msaada wowote kama ilivyodhihirika katika ripoti ya majanga asili duniani iliyowasilishw amjini Berlin. Rudolf Seiters ni kiongozi wa shirika la msalaba mwekundu tawi la Ujerumani.

´Habari kutoka maeneo yaliyosahaulika ambayo yako katika hali mbaya baada ya kukumbwa na majanga asili ni jambo linalowavutia walimwengu na vyombo vya habari.´

Jambo hili linapata nafasi ndogo katika matumizi ya michango inayotolewa kuwasaidia wahanga wa majanga duniani. Kwa waathiriwa wa janga la tsunami kusini mwa Asia, mkasa ulioripotiwa sana na vyombo vya habari, yuro 933 zimemfikia kila muhanga kama msaada. Kwa wahanga wengine wa majanga nchini Chad au Guyana ni kiasi cha yuro 20.

Mtangazaji mashuhuri wa runinga moja hapa Ujerumani Maybit Illner aliyehudhuria mkutano wa kuwasilishwa kwa ripoti kama balozi wa shirika la msalaba mwekundu aliuliza,

´Kwa nini kimbunga Katrina nchini Marekani kilichowaua watu 1,300 kiliripotiwa zaidi katika vyombo vya habari kuliko kimbunga Stan kilichotokea muda mfupi baadaye na kuua watu 1,600 nchini Guatemala?´

Jawabu la ripoti ya shirika la msalaba mwekundu kwamba majanga yanayozusha hisia kubwa zaidi ni yale yanayosababisha athari kubwa halitoshelezi. Mfumo mzuri wa vyombo vya habari una jukumu kubwa na muhimukwani katika maeneo yanaykumbwa na majanga vyombo vya habari vinaweza kutuma picha katika runinga na ripoti kwa gharama ndogo. Maybit Illner anafahamu pia kwamba utawala wa kiimla katika baadhi ya maeneo huzuia ripoti kutolewa kutoka maeneo yaliyoathiriwa na majanga asili.

Ripoti ya majanga duniani imedhihirisha kuongezeka kwa majanga. Watu milioni 161 waliathiriwa huku wengine takriban laki moja wakafariki dunia. Idadi ya waathiriwa wa mafuriko imeongezeka kwa asilimia 50 na kwa shirika la msalaba mwekundu hiyo ni ishara ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani, Heidermarie Wieczorek-Zeul alisema ipo haja ya kufanya juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, njia mojawapo ikiwa ni matumizi yla nishati endelevu. Aidha alisema kuyalinda mazingira na maeneo yenye misitu zitakuwa mada muhimu zitakazojadiliwa kwenye mkutano wa mataifa ya G8 na halmashauri ya Umoja wa Ulaya katika majuma machache yajayo.

Ripoti ya msalaba mwekundu pia ilizunguzia juu ya tatizo la njaa na magonjwa. Waziri Heidermarie Wieczorek Zoel alisema watu 8,000 wanaofariki dunia kila siku kutokana na ukimwi ni janga kwa jamii husika na nchi zinazokabiliwa. Na kwa kuwa majanga yaliyosahaulika ni mada kuu katika ripoti ya shirika la msalaba mwekundu Wieczorek Zeul alisema jamii ya kimataifa haitakiwi tu kuzungumzia mashaka ya raia wa jimbo la Darfur bali inatakiwa kuchukua hatua na kuumaliza mzozo wa Darfur.

Shirika la msalaba mwekundu tawi la Ujerumani kama kiongozi wake Rudolf Seiters, linataka katika siku za usoni kuwashughulikia zaidi wahanga wa majanga yaliyosahaulika.