1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makombora ya Korea Kaskazini yazidi kuitisha Japan

Isaac Gamba
8 Agosti 2017

Waraka wa muongozo wa ulinzi  wa Japan uliochapishwa unaonesha kuwa kitisho kinacho sababishwa na Korea Kaskazini sasa kimefikia hatua nyingine mpya kutokana na Korea Kaskazini sasa kuwa na uwezo wa kufyatua makombora.

https://p.dw.com/p/2hr4K
USA Besuch Shinzo Abe in Washington
Picha: picture-alliance/dpa/A. Harnik

Japan kupitia katika  waraka huo wa kila mwaka  unaohusiana na masuala ya ulinzi uliotolewa Jumanne imetoa onyo juu ya  kitisho cha Korea Kaskazini kinachotokana na mipango yake ya silaha za nyukilia.

Licha ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa vilivyowekwa dhidi ya nchi hiyo Korea Kaskazini imeendeleza majaribio yake ya makombora  ikiwa ni pamoja na kufyatua makombora  mawili ya kutoka bara moja kwenda jingine mwezi uliopita  ambayo yalifika katika kisiwa cha Hokkaido magharibi mwa Japan.

Tangu mwaka jana wakati Korea Kaskazini ilipofanya majaribio mawili ya makombora ya nyukilia na  makombora mengine 20 ya masafa marefu kitisho dhidi  ya usalama kinaonekana kuchukua sura mpya. Umesema waraka huo wa  wizara ya ulinzi ya Japan wenye kurasa 563.

Inafikiriwa  kuwa mpango wa silaha za nyukilia wa Korea Kaskazini tayari umepiga hatua kubwa na huenda taifa hilo likawa  tayari na makombora ya kinyukilia.

Majaribio ya hivi karibuni yaliyofanywa na Korea Kaskazini kwa kufyatua  makombora ya kutoka bara moja kwenda jingine yanaonesha kuwa makombora hayo yanaweza kufika umbali  mrefu  zaidi ya Japan na pia kufika  Marekani.

Japan yachukua hatua za tahadhari

Japan neuer Verteidigungsminister Itsunori Onodera
Itsunori Onodera waziri mpya wa ulinzi wa JapanPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Kambayashi

Kuongezeka kwa kitisho cha Korea Kaskazini kumeifanya Japan kuchukua hatua za tahadhari ikiwa ni pamoja na mazoezi kadhaa ili kujiweka tayari iwapo kutatokea shambulizi lolote.

Kufuatia hatua ya Korea Kaskazini kuendelea na majaribio yake ya makombora kundi la wabunge kutoka chama tawala nchini Japan likiongozwa na Itsunori Onodera aliyateuliwa kuwa waziri wa ulinzi Alhamisi iliyopita lilimtaka Waziri Mkuu wa Japan  Shinzo Abe mwezi Machi kufikiria juu ya kuchukua hatua za kushambulia maeneo ya maadui hatua ambayo hata hivyo itaonekana kuwa ni mwelekeo mpya katika sera nje za Japan kuhusiana na masuala ya ulinzi.

Wakati serikali ya sasa ya Japan katika miaka ya hivi karibuni imepitia upya katiba ya nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti yake ya ulinzi hajawahi kufikiria kuwa na ndege za kivita au makombora  ya masafa ya kutosha yenye uwezo wa kusambulia mataifa mengine.

Aidha waraka huo uliotolewa na  wizara ya ulinzi ya Japan unaelezea juu ya hatua ya China kuzidi kujiimarisha katika ukanda huo ikigusia idadi ya ndege za kivita za Japan kulinganisha na China huku kukiwa na uwezekano kuwa shughuli zinazohusiana na na masualaya ulinzi katika ukanda wa bahari pamoja na zile za anga zinaweza kuongezeka katika ukanda wa bahari ya Japan kuanzia sasa.

Mahusiano ya Japan na China yameoneka kuzorota katika miaka ya hivi karibuni kutokana na mzozo wa visiwa visivyokaliwa na watu katika bahari ya China mashariki.

Wakati huohuo Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson amewasili Bangkok Thailand hii leo akiwa na wito wa kuitaka nchi hiyo ya kifalme kusitisha mahuasiano yake ya kibiashara na Korea Kaskazini ikiwa ni hatua ya  Marekani  za kuwashawishi washirika wake kuunga mkono juhudi zake za kuitaka Korea Kaskazini kuachana na malengo yake ya kuwa na silaha za nyukilia.

Thailand ni moja ya nchi za kusini mashariki mwa Asia  zilizo na ofisi za ubalozi wa Korea Kaskazini na ina mahusiano mazuri ya kibiashara na Korea Kaskazini.

Kwa mujibu wa Suzan Thornton ambaye ni afisa wa Marekani anayehusika na masuala ya mashariki mwa Asia  Tilleson analenga kuishawishi Thailand  kuyadhibiti makampuni ya Korea Kaskazini yaliyoko nchini humo yanayotumia nafasi hiyo kzid kujiimarisha kibiashara.

Mwandishi: Isaac Gamba

Mhariri: Iddi Ssessanga