1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majenerali wanamtii nani nchini Misri?

Oumilkher Hamidou31 Januari 2011

Nafasi inayoshikiliwa na jeshi katika kudhamini nidhamu nchini Misri.Na eti kweli jeshi linaweza kuamua mustakbal wa rais Hosni Mubarak?

https://p.dw.com/p/107xs
Polisi wawatimua waandamanajiPicha: AP

Maandamano ya umma katika miji kadhaa ya Misri yameutikisa vibaya sana utawala wa rais Hosni Mubarak hadi kufikia ukingoni mwa kuporomoka.Mubarak ambae ni mkuu wa vikosi vya wanajeshi amehisi analazimika kulitumia jeshi ili kurejesha utulivu na nidhamu.Lakini jeshi limejiweka nyuma kabisa -hali inayosifiwa na kushukuriwa na waandamanaji.Jeshi linaweza kushikilia nafasi muhimu katika kinyang'anyiro cha kuania madaraka nchini Misri-Suala linalozuka lakini ni nafasi gani.

Mkuu huyo wa zamani wa jeshi la wanaanga,ambae pia ndie mkuu wa vikosi vya wanajeshi vya Misri,Hosni Mubarak,anaitawala nchi hiyo tangu miaka 30 iliyopita akitangaza sheria ya hali ya hatari.Hadi ghadhabu hizi za sasa za umma ziliporipuka,jeshi lilikuwa likiangaliwa kama mhimili muhimu wa utawala wake.Lakini ghadhabu za ghafla za umma zimemlazimisha rais sio tuu aivunje serikali ambayo tokea hapo ilikuwa ikionyesha imezidiwa,lakini pia akawakabidhi vyeo vya juu madarakani wale watu anaowaamini.

Ägypten Proteste Chaos
Picha ya Mubarak yapigwa kiatuPicha: dapd

Kuhusu suala nafasi gani inashikiliwa na jeshi katika kinyang'anyiro cha kuania madaraka nchini Misri-hapo hoja zinatofautiana-kuna wanaosema ushawishi mkubwa wa wanajeshi unatokea Washington.Kuna wanaojiuliza kama jeshi litaendelea kumtii Mubarak licha ya kuchukiwa na wananchi na licha ya shinikizo la kimataifa?Tallat Musallam,jenerali wa zamani na ambae pia ni mtaalam wa masuala ya kijeshi mjini Cairo haamini hilo.Analiangalia jeshi kama mlinzi wa taifa anasema:

"Jukumu la mwanzo kabisa la jeshi la Misri ni kudhamini nidhamu na sio kuunga mkono kundi hili au lile la kisiasa.Matukio ya jana na leo yamedhihirisha wazi kabisa vikosi vya wanajeshi havijaitika ipasayo amri ya viongozi wa kijeshi.Ndio maana,siamini mie kama wanajeshi watamuunga mkono rais Mubarak."

Proteste in Ägypten gegen Mubarak Regime gehen weiter Tahrir Square Platz Kairo
Waandamanaji katika uwanja wa Tahriri mjini CairoPicha: picture-alliance/dpa

Vifaru vinalinda majengo muhimu ya serikali mjini Cairo,mfano kituo cha televisheni katika eneo la mto Nil,makumbusho ya taifa na kasri la rais.Viongozi wa kijeshi wanajaribu kuinusuru nchi hiyo isitumbukie katika janga la vurugu na fujo baada ya polisi ambao hawapendwi kushindwa hivi karibuni kuidhibiti hali ya mambo.Kuanzia jumapili iliyopita jeshi limepelekwa pia kulinda eneo linalowavutia watalii-Charm al Sheikh katika bahari ya Sham.

Wanajeshi nchini Misri wanajivunia sifa nzuri kinyume na vikosi vya polisi vinavyotuhumiwa kupokea rushwa.

Katika zilzala hii ya kisiasa inayopiga nchini Misri wadadisi wa kisiasa wanakubaliana juu ya kitu kimoja:majemedari wana nguvu za kutosha kuweza kuamua hatima ya Hosni Mubarak.Kuna wanaofika hadi ya kuzungumzia uwezekano wa kuundwa serikali ya mpito itakayoongozwa na jeshi.

Mwandishi:Mudhoon Loay/Dw Arabisch/Hamidou Oummilkheir

Mpitiaji:Abdul-Rahman