1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Afghanistan waukomboa mji wa Kunduz

1 Oktoba 2015

Majeshi ya Afghanistan yameyakomboa maeneo muhimu ya mji wa Kunduz kutoka kwa wanamgambo wa Taliban baada ya wanamgambo hao kuudhibiti kwa siku tatu mfululizo.

https://p.dw.com/p/1GgNs
Picha: picture-alliance/dpa/J. Karger

Wanajeshi wa Afghanistan ambao walitatizwa na kuchelewa kwa wanajeshi zaidi lakini walipigwa jeki na mashambulizi ya angani yaliyofanywa na jeshi la Marekani yamefanikiwa kuukomboa mji wa Kunduz ambao ni mji mkuu wa jimbo la Kunduz lililoko kaskazini mwa Afghansitan.

Wakaazi wa mji huo wamesema wanajeshi waliweza kufika kati kati ya mji huo hii leo ambapo barabara zimetapakaa miili ya wanamgambo wa Taliban na kuongeza mapigano bado yanaendelea katika baadhi ya sehemu za mji huo. Wakaazi hao wa Kunduz wamemiminika mitaani kusherehekea ushindi huo wa wanajeshi wao na kuwashukuru.

Taliban wafurushwa Kunduz

Msemaji wa wizara ya ulinzi Dawlat Waziri amesema wanamgambo wa Taliban wameondoka mjini Kunduz na operesheni ya safisha safisha inaendelea. Matamshi ambayo pia yamethibitishwa na mkuu wa polisi wa Kunduz Qasim Jangal Bangh. Taarifa kutoka wizara hiyo ya ulinzi imesema wanamgambo 150 wameuawa na wengine 90 wamejeruhiwa katika operesheni hiyo iliyofanywa usiku kucha.

Maafisa wa usalama wa Afghanistan wakiwasili Kunduz
Maafisa wa usalama wa Afghanistan wakiwasili KunduzPicha: Reuters

Hata hivyo msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid amekanusha kuwa wanajeshi wameukomboa mji wa Kunduz na kusema wapiganaji wake bado wanapambana na wanajeshi na bado wanayadhibiti maeneo mengi ya mji huo.

Maafisa wa usalama wamesema wanamgambo hao wa Taliban waliingia mjini humo wakati wa sherehe zilizokamilika hivi punde za Eid na kufanya mashambulizi makali yaliyowawezesha kuudhibiti baada ya saa chache ya mapambano siku ya Jumatatu.

Kudhibitiwa kwa mji huo wa Kunduz kulisadifiana na kuadhimishwa mwaka mmoja tangu serikali ya muungano inayoongozwa na Rais Ashraf Ghani kuingia madarakani.

Shambulizi hilo la Taliban na kuudhibiti mji wa Kunduz ambao ndiyo mji mkuu wa kwanza wa jimbo nchini Afghansitan kudhibitiwa kikamilifu na wanamgambo hao katika kipindi cha miaka kumi na nne iliyopita tangu kung'olewa madarakani na wanajeshi wa Marekani kunadhihirisha kuwa bado eneo la kaskazini mwa nchi hiyo liko katika hatari ya kutaliwa na wanamgambo.

Taliban bado ni kitisho

Mchambuzi wa masuala ya kijeshi mjini Kabul Atiqullah Amarkhil amesema wanamgambo wa Taliban wanafahamu kuwa hawana uwezo wa kuudhibiti mji mkubwa kama Kunduz lakini kuudhibiti hata japo kwa siku chache, kunadhihirisha kuwa wana nguvu na hivyo kuwa na usemi katika mazungumzo ya kutafuta amani kati yao na serikali.

Mmoja wa wanamgambo wa Taliban akizungumza na mkaazi wa Kunduz
Mmoja wa wanamgambo wa Taliban akizungumza na mkaazi wa KunduzPicha: Reuters

Kudhibitiwa kwa mji huo miezi tisa tu baada ya majeshi ya jumuiya ya kujihami ya NATO kukamilisha operesheni yao nchini humo na kubakisha wanajeshi 13,000 pekee, kunaibua wasiwasi kuhusu uwezo wa majeshi ya Afghanistan kupambana kivyao dhidi ya Taliban.

Hata baada ya miaka kadhaa ya kupewa mafunzo na kununuliwa kwa silaha ambapo Marekani imetumia takriban dola bilioni 65 kuwapa uwezo wanajeshi wa Afghanistan,wanajeshi hao wameshindwa kuwadhibiti kikamilifu wanamgambo hao na kuibua mashaka iwapo Marekani iwaondoe wengi wa wanajeshi wake au la kutoka Afghanistan ifikapo mwaka ujao.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri:Josephat Charo